SYRIA-KERRY-USALAMA

Kerry: hali nchini Syria "inatisha"

Sergueï Lavrov (kushoto) na John Kerry, Machi 2, 2015 Geneva.
Sergueï Lavrov (kushoto) na John Kerry, Machi 2, 2015 Geneva. REUTERS/Evan Vucci/Pool

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry, ziarani mjini Geneva, uswisi ameelezea wasi wasi wake kuhusu hali inavyoendelea nchini Syria. John Kerry, katika mkutano na vyombo vya habari, amesema hali nchini Syria "inatisha".

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza baada ya kukutana kwa mazungumzo na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Staffan de Mistura, Bw Kerry ameongeza kuwa angelimuita kwa njia ya simu baadaye Jumatatu hii mchana mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov kwa kumshawishi kwa ajili ya kusimamishwa kwa mapigano.

Hata hivyo, Kerry ameonya kuwa hakutaka kuahadi mafanikio.

Bw Kerry pia amemshukuru Bw de Mistura, kwa msaada wa mchakato wa kisiasa wakati ambapo nchi hiyo bado inakabiliwa na "mgogoro ambao kwa sasa umeshindikana kudhibitiwa na ambao umekua ni mzigo kwa kila mmoja duniani ."

Kerry ameongeza kuwa mkataba wa usitishwaji mapigano chini ya upatanishi wa Urusi na Marekani mwezi Februari ulikua bado ukiheshimishwa, isipokuwa katika jimbo la Aleppo.

Katika Jimbo la Aleppo, Kerry amesema, serikali ya Syria imeendesha mashabulizi kwa makusudi katika vituo vitatu vya afya na hospitali moja kubwa, na kuua madaktari na wagonjwa.

"Mashambulizi dhidi ya hospitali ni kitendo kisichoeleweka" na "jambo hili ambalo linapaswa kukoma," John Kerry amesema.

Zaidi ya watu 250, ikiwa ni pamoja na watoto hamsini wameuawa tangu kuanza tena kwa mapigano Aprili 22 katika jimbo la Aleppo, wengi wameuawa katika mashambulizi ya anga ya jeshi la serikali, katika ukiukaji wa mkataba wa usitishwa mapigano.

"Pande zote mbili, upinzani na serikali, zimechangia katika machafuko hayo, na tutafanya kazi katika masaa yajayo kujaribu kurejesha hali ya utulivu na kuzisihi pande zote mbili kuheshimu mkataba wa usitishwaji mapigano," amesema Kerry.

"Tunaandaa utaratibu mzuri, lakini tunahitaji utashi wa kisiasa," ameongeza, bila kutoa maelezo zaidi.