MAREKANI-TRUMP

Trump atengua matamshi yake dhidi ya Waislam

Mgombea urais katika kura za mchujo kwa chama cha Republican, Donald Trump, katika kampeni Eugene katika jimbo la Oregon, Mei 6, 2016.
Mgombea urais katika kura za mchujo kwa chama cha Republican, Donald Trump, katika kampeni Eugene katika jimbo la Oregon, Mei 6, 2016. REUTERS/Jim Urquhart

Mgombea urais kupitia chama cha Republican nchini Marekani Donald Trump ameonekana kulegeza msimamo wake kuhusu ujio wa Waislamu nchini Marekani ikiwa atachaguliwa kura rais.

Matangazo ya kibiashara

Bwana Trump amesema kuwa kauli yake ya hapo awali ilikuwa ni mapendekezo tu.

Trump amesema hayo baada ya Meya mpya wa jiji la London ambaye ni Mwislamu Sadiq Khan, kusema kuwa hataweza kwenda Marekani ikiwa Trump atakuwa rais wa nchi hiyo.

Pendekezo la kuwazuia waislamu kuingia nchini Marekani lilipata upinzani mkubwa ndani na nje ya Marekani.

Wizara ya ulinzi ya Marekani ilisema matamshi ya Donald Trump kwamba Waislamu wanafaa kuzuiwa kuingia Marekani ni hatari kwa usalama wa taifa la Marekani na raia wake.

Pentagon imesema matamshi hayo yatasaidia kundi linalojiita Islamic State (IS) kuendeleza harakati zake dhidi ya Marekani na raia wake.

Trump, ambaye anaongoza katika kinyang’anyiro cha kumteua mgombea urais Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, alitoa matamshi hayo baada ya watu 14 kuuawa kwa kupigwa risasi mjini San Bernardino, California.