MAREKANI-OBAMA-HIROSHIMA

Obama Hiroshima: ziara ya kihistoria

Eneo la kumbukumbu kulikorushwa bomu la nyuklia Agosti 6, 1945 Hiroshima, na kusababisha vifo vya watu 140,000.
Eneo la kumbukumbu kulikorushwa bomu la nyuklia Agosti 6, 1945 Hiroshima, na kusababisha vifo vya watu 140,000. Reuters

Barack Obama anatazamiwa kuzuru mji wa Hiroshima Ijuma hii Mei 27 nchini Japan. Hata hivyo Bw Obama, hivi karibuni aliliambia shirika la serikali la utangazaji la Japan NHK kuwa hatoomba msamaha katika tukio hilo.

Matangazo ya kibiashara

Hii ni ziara ya kwanza kwa rais wa Marekani kwenye eneo kulikotokea mlipuko wa bomu la kwanza la atomiki lililorushwa Agosti 6,1945 na kuua watu 140,000. Ikulu ya White House inasema haimaanishi kuwa Barack Obama ataomba msamaha.

Ziara hii ya kihistoria imekua ikiandaliwa kwa miezi kadhaa. Ingawa Barack Obama hajawahi kuomba msamaha wakati wa ziara yake kufuatia mkasa uliyoukumba mji wa Hiroshima, uwepo wake kwenye eneo kulikotokea mlipuko wa kwanza wa bomu la atomiki unaweza kutafsiriwa kwa maoni mbalimbali nchini Marekani. Kwa mujibu wa Ikulu ya White House, rais wa Marekani atatoa hotuba akionyesha ahadi yake kwa dunia isiyokua na silaha ya nyuklia.

Akitembelea Hiroshima mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, alifungua njia kwa baraka za rais. Zoezi hili pengine litakaribishwa kimataifa, lakini ni hatari katika suala la sera za ndani kwa Barack Obama, ambaye ataondoka Ikulu ya White House mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa upande wake, chama Republican ambacho kinaendelea na kampeni zake za uchaguzi wa urais, kwa miezi kadhaa kimekua kikimkosoa "rais ambaye amedhoofisha Marekani kwa kuomba msamaha."

Obama atajitahidi kutumia maneno mazuri ili asiwezi kuwakosea maveterani wa Marekani waliopigana katika vita vya Marekani dhidi ya Japan.