MAREKANI-MUHAMMAD ALI

Ibada ya maombi yafanyika kwa kumkumbuka Muhammad Ali

Mwanamasumbwi Muhammad Ali, ambaye mazishi yake yatafanyika Ijumaa Juni 10.
Mwanamasumbwi Muhammad Ali, ambaye mazishi yake yatafanyika Ijumaa Juni 10. Reuters/路透社

Maelfu ya raia kutoka mataifa mbalimbali duniani, wameshirikI kwenye maombi ya pamoja ya kiislamu, kumkumbuka, Muhammad Ali, nguli wa masumbwi, aliyefariki juma moja lililopita.

Matangazo ya kibiashara

Maombi haya yaliyofanyika kwenye msikiti wa Louisville, alikozaliwa Muhammad Ali na kuishi huko kwa muda mrefu, yalikuwa ni sehemu ya ibada ya siku mbili ya kumkumbuka na kutoa heshima za mwisho kwa mwanamasumbwi huyu aliyekuwa kipenzi cha dunia, na shujaa aliyetetea haki za binadamu.

Wanaume, wanawake na mamia ya familia walifurika kwenye ukumbi wa Freedom, mjini Kentucky kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa marehemu Muhammad Ali kabla ya maziko yanayotarajiwa kufanyika hii leo.

Sherehe fupi iliyofanyika kwenye mji wa Louisville, ilikuwa ni sehemu ya kuzindua siku mbili za ibada za pamoja kwa dini ya kiislamu na Kikristo kama alivyotaka kufanyika marehemu muhammad Ali kabla ya kufariki kwake.

Imamu aliyeoongoza ibada ya kumuombea Muhammad Ali, amesema kuwa alifurahishwa kuona watu wa mataifa mbalimbali wakikusanyika bila kujali tamaduni, rangi, dini wala itikadi na kwamba ulikuwa ni wakati muafaka kukumbuka mazuri aliyoyafanya mwanamasumbwi huyu.

Hii leo ibada ya mazishi itafanyika, ambapo viongozi kadhaa wa dunia wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Ali aliyefariki akiwa na umri wa miaka 74, ambapo anatajwa na kila raia kuwa alikuwa mtu wa aina yake.