SIASA-MAREKANI

Hillary Clinton aweka historia baada ya kuteuliwa na chama chake

Hillary Clinton ameweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuidhinishwa kuwa mgombea urais katika historia ya nchi ya Marekani.

Wajumbe walivyopokea kuteuliwa kwa  Hillary Clinton kuwa mgombea urais kupitia chama cha Democratic Julai 26 2016
Wajumbe walivyopokea kuteuliwa kwa Hillary Clinton kuwa mgombea urais kupitia chama cha Democratic Julai 26 2016 REUTERS/Rick Wilking
Matangazo ya kibiashara

Ni rasmi sasa kuwa Seneta huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 68, atapambana na mgombea wa Republican Donald Trump wakati wa uchaguzi mkuu mwezi Novemba mwaka huu.

Clinton alihitaji wajumbe 2,382 kuidhinishwa kwa mgombea wa Democratic, idadi ambayo iliipata baada ya kupitishwa na wajumbe wote.

Baada ya uteuzi huo rais wa zamani na mume wa mgombea huyo Bill Clinton, aliwahotubia maelfu ya wajumbe hao katika mkutano huo unaoendelea kwa siku ya tatu leo katika mji wa Philadelphia.

Rais wa zamani Bill Clinton akihotubia wajumbe wa chama cha Democratic Julai 26 2016
Rais wa zamani Bill Clinton akihotubia wajumbe wa chama cha Democratic Julai 26 2016 theglobeandmail

Rais huyo wa zamani amemwelezea mkewe kama mtu aliye na uwezo mkubwa kuongoza na kuibadilisha nchi hiyo.

Aidha, aliwaambia wajumbe hao namna alivyoanza urafiki, uchumba na kumuuoa Hillary miaka ya 70 baada ya kukutana chuoni.

Leo itakuwa zamu ya Rais Barrack Obama na Makamu wake Joe Biden, na mgombea mwenza wa Bi.Clinton Tim Kaine, kuwahotunia wajumbe hao.

Hillary Clinton naye anatarajiwa kuwa mzungumzaji wa mwisho hapo kesho atakapokubali uteuzi huo.