MDAHALO WA URAISI-MAREKANI

Trump amshambulia Clinton kuhusu mume wake kwenye mdahalo televisheni

Wagombea urais nchini Marekani, Donald Trump wa Republican na Hillary Clinton wa Democrat, wakionekana kwenye picha wakijibizana wakati wa mdahalo wao wa pili wa Televisheni uliofanyika October 9, 2016.
Wagombea urais nchini Marekani, Donald Trump wa Republican na Hillary Clinton wa Democrat, wakionekana kwenye picha wakijibizana wakati wa mdahalo wao wa pili wa Televisheni uliofanyika October 9, 2016. REUTERS/Jim Young

Mgombea urais nchini Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican, Donald Trump, amejitetea dhidi ya matamshi yake ya kibaguzi aliyowahik kuyatoa dhidi ya wanawake, badala yake akamshambulia mpinzani wake Hillary Clinton na mume wake Bill Clinton.

Matangazo ya kibiashara

Mgombea huyu wa Republican amekanusha vikali kufanya vitendo vya udhalilishaji wa kingono dhidi ya wanawake, badala yake aliamua kutumia nafasi aliyopewa kukanusha tuhuma dhidi yake kumshambulia Clinton na familia yake.

“Hakuna mtu yeyote katika historia ya siasa za Marekani ambaye amekuwa mdhalilishaji dhidi ya wanawake,” alisema Trump.

Hata hivyo katika kile ambacho wachambuzi wa mambo walikitarajia, Hillary Clinton aliamua kutojibu wa kufafanua tuhuma zozote zilizoelekezwa kwake na Donald Trump dhidi ya mume wake.

Mashambilizi ya Trump dhidi ya familia ya Clinton, yalianza wakati mmoja wa waongoza mjadala wa hivi leo, Anderson Cooper kumuuliza kuhusu video iliyorekodiwa mwaka 2005 na kuchapishwa juma lililopita, ikimuonesha Trump akitoa matamshi ya kejeli dhidi ya wanawake.

Lakini aliposhinikizwa zaidi kujibu swali ikiwa aliwahi kujihusisha kingono na mwanamke yeyote, alikanusha kufanya kitendo hicho na badala yake akarejesha tuhuma zilizokuwa zikimkabili Bill Clinton kuhusu wanawake aliodaiwa kuwadhalilisha.

Hata hivyo hakuna mashtaka yoyote yaliyowasilishwa mbele ya mahakama kuhusu vitendo vya udhalilishaji wa kingono vilivyowahi kufwanya na Clinton wakati akiwa rais.

Hillary Clinton hata hivyo akatumia mwanya huo, kumuelezea namna ambavyo mpinzani wake anawachukulia wanawake, akitolea mfano picha za video zilizotolewa juma lililopita na kusababisha baadhi ya wanachama wa juu kwenye chama chake cha Republican kutangaza kujiondoa kumuunga mkono.

Hata hivyo kwa mara ya kwanza wagombea wote wawili kila mmoja alipewa nafasi ya kumuelezea mwenzake, huku Clinton akisifu namna ambavyo Trump amewalea watoto wake na kuwa mfano, huku Trump akimuelezea Clinton kama mwanamke shupavu asiyeshindwa wala kukata tamaa.

Mdahalo mwingine wa televisheni ambao utakuwa ni wa mwisho kati ya midahalo mitatu iliyopangwa, utafanyika October 19 mwaka huu, ambapo wagombea hao watakuwa na fursa ya mwisho kuwashawishi wapiga kura wa Marekani kabla ya uchaguzi mkuu wa tarehe 8 November mwaka huu.