COLOMBIA-ELN

Colombia: Kuelekea mazungumzo ya amani kati ya waasi wa ELN na utawala

Waasi wa kundi la ELN wakipiga doria katika eneo wanalodhibiti mwaka 2000.
Waasi wa kundi la ELN wakipiga doria katika eneo wanalodhibiti mwaka 2000. AFP PHOTO STR

Huenda inaweza kuwa mwisho wa zaidi ya nusu karne ya vita nchini Colombia hivi karibuni. Kundi la waasi wa ELN na serikali ya Colombia wametangaza kuwa walifikia makubaliano Jumatatu wiki hii nchini Venezuela.

Matangazo ya kibiashara

Baada ya kushinda Tuzo ya amani ya Nobel Ijumaa juma lililopita kwa jitihada zake katika mchakato wa amani na kundi la waasi la FARC, rais Juan Mauel Santos ana matumaini ya kufikia makubaliano ya amani na kundi la waasi la ELN.

Kundi la waasi la ELN na serikali ya Colombia wamesema kuwa wataanza hadharanimazungumzo ya amani tarehe 27 Oktoba katika mji wa Quito, nchini Ecuador.

Hatua ya kwanza ya makubaliano kati ya pande hizo mbili ambayo itajadiliwa katika mkutano wa mjini Quito mwishoni mwa mwezi huu ni kushiriki kwa jamii nzima ya wananchi wa Colombia katika mchakato wa amani na kundi la pili la waasi nchini.

Tanagazo hili huenda ni ushindi kwa Juan Manuel Santos siku nane baada ya kupata pigo kubwa baada ya kukataliwa makubaliano ya amani yaliyoafikiwa na kundi la waasi la FARC katika kura ya maoni iliyopigwa Oktoba 2 mwaka huu.

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos amesema ana matumaini ya 'kufikia amani kamili' na kundi la waasi la ELN. Kamili kwa sababu kundi la waasi la ELN liko pamoja na kundi kuu la waasi la FARC. Kundi hili la waasi la ELN lilianzishwa katika miaka ya 60, na lina wapiganaji 1,500.