MAREKANI-SIASA

Donald Trump ashinda urais nchini Marekani

Trump alipata ushindi wa kura za wajumbe  274 na kumshinda Bi. Clinton aliyepata kura 215.

Rais mteule wa Marekani Donald Trump
Rais mteule wa Marekani Donald Trump REUTERS/Carlo Allegri
Matangazo ya kibiashara

Akiwahotubia wafuasi wa chama cha Republican jijini New York, Trump amesema atakuwa rais wa Wamarekani wote na kusema anatambua kazi kubwa aliyonayo ya kuliunganisha tena taifa hilo.

"Nitakuwa rais wa raia wote wa Marekani," amesema Trump.

Aidha, amesema amezungumza na Bi.Clinton ambaye amempongeza kwa ushindi aliopata katika uchaguzi huu.

"Nimezungumza na Bi.Clinton na amenipongeza kwa ushindi huu. Nampongeza sana kwa ushindani alionipa katika uchaguzi huu.

Clinton ameifanyia nchi hii  kazi kubwa na tuna deni kubwa sana kwake," amesema Trump.

Rais huyo mteule ameahidi kuimarisha uchumi wa taifa hilo na kuunda nafasi za kazi kwa raia wa Marekani na kurejesha heshima ya Marekani duniani.

Kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Mataifa mengine ya dunia, Trump amesema pamoja na maslahi ya Marekani kuwa mstari wa mbele, atahakikisha kuwa anafanya kazi vizuri na kwa usawa na mataifa yote yatakayokuwa tayari kushirikiana naye.

"Sitawaangusha.Nitahakikisha kuwa nakuwa rais bora kwenu," amewaambia maelfu ya wafuasi wa Republican waliokuwa wanamsheherekea.

Trump anatarajiwa kuapihswa mwezi Januari na kuwa rais wa 45 wa Marekani.