MAREKANI

Obama kukutana na Trump Ikulu ya Marekani

Ikulu ya Marekani jijini Washington DC
Ikulu ya Marekani jijini Washington DC media-cache

Rais wa Marekani Barrack Obama anatarajiwa kumpokea rais mteule Donald Trump katika Ikulu ya White House baadaye siku ya Alhamisi jijini Washington DC.

Matangazo ya kibiashara

Obama na Trump wanatarajiwa kuzungumzia namna ya kupokezana uongozi wa nchi hiyo kwa njia mwafaka, kama ilivyokuwa kwa Obama wakati akichukua uongozi kutoka kwa mtangulizi wake George W Bush mwaka 2008.

Trump anatarajiwa kuapishwa tarehe 20 mwezi Januari mwakani, na kuwa rais wa 45 wa taifa hilo lenye nguvu duniani baada ya kuibuka mshindi wa uchaguzi wa nchi hiyo.

Siku ya Jumatano, rais Obama aliwataka Wamarekani kuyakubali matokeo hayo na kumpa Trump nafasi kuongoza taifa hilo baada yake.

Bi.Clinton naye alikuwa na ujumbe kama huo na kuwaambia raia wa Marekani hasa wafuasi wake kuyakubali matokeo hayo na kuungana na Trump ili kufanikisha uongozi wake.

Wachambuzi wa siasa wanasema, Trump sasa ana kazi kubwa ya kuliunganisha tena taifa hilo na kumaliza mvutano wa kisiasa nchini humo.