MAREKANI

Wabunge wa Republican wabadili aumuzi wao kuhusu kamati ya maadili

Wawakilishi wa chama cha Republican nchini Marekani, hatimaye wameachana na mpango wa kuipunguzia mamlaka kamati huru ya maadili iliyokuwa na jukumu la kuchunguza makosa ya kinidhamu yanayofanywa na wanasiasa, hatua iliyokuja baada ya baadhi yao kutofautiana.

Wabunge nchini Marekani wakiwa katika kikao chao cha kwanza, 3 Januari 2017
Wabunge nchini Marekani wakiwa katika kikao chao cha kwanza, 3 Januari 2017 REUTERS/Jonathan Ernst
Matangazo ya kibiashara

Uamuzi wa wabunge wa Republican kutaka kuiondolea baadhi ya mamlaka tume hiyo ya maadili, ulisababisha ukosolewaji mkubwa, hatua iliyopingwa pia na rais mteule Donald Trump.

Akiandika kupitia kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter, Trump aliandika "Jikiteni kwenye mabadiliko ya sheria za kodi, afya na mambo mengine mengi yenye tija kwa wananchi!" alisema Trump.

Uamuzi huu wa siri, ambao uligubika kikao cha kwanza cha 115 cha bunge la Congress, ulibadilishwa baada ya kuitishwa kwa kikao cha dharura.

Kamati ya maadili iliundwa mwaka 2008 baada ya kuibuliwa kwa tuhuma mbalimbali za kimaadili dhidi ya wabunge na baadhi yao kujikuta wakihukumiwa kifungo gerezani.

Rais mteule Trump tayari ameweka wazi msimamo wake wa kupambana na vitendo vya rushwa kama alivyoainisha kwenye kampeni zake za kuingia ikulu, akiapa kudhibiti mianya yote ya rushwa.

Spika wa bunge toka chama cha Republican Paul Ryan ambaye amechaguliwa tena kwenye wadhifa huo, alijaribu kuwashawishi wabunge hao bila mafanikio, ambapo ulipitishwa kwa kura nyingi kabla ya uamuzi huo kubatilishwa.