MAREKANI

Trump kufanya maamuzi magumu kuhusu usalama na uhamiaji

Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumatano ni siku kubwa kwa raia wa nchi yake kuhusu maswala ya usalama.

Rais wa Marekani  Donald Trump, akiwa kazini katika Ikulu ya White House
Rais wa Marekani Donald Trump, akiwa kazini katika Ikulu ya White House REUTERS/Kevin Lamarque
Matangazo ya kibiashara

Trump anatarajiwa kutia saini maamuzi kadhaa ya rais kuanza kutekelezwa kuhusu usalama wa nchi hiyo lakini pia suala tata la uhamiaji.

Kiongozi huyo anatarajiwa kutangaza kuwa Mexico itaanza kugharamia ujenzi wa ukuta katika mpaka wake ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu wanaokuja Marekani.

Aidha, agizo la rais Trump linatarajiwa pia kuweka mazingira magumu ya kupata visa kwa raia wa mataifa kadhaa kutoka Mashariki ya Kati na bara la Afrika.

Mataifa yanayotajwa ni pamoja na Syria, Yemen, Iraq, Somalia na Sudan.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema “Ni siku kubwa kuhusu usalama wa nchi. Miongoni mwa mambo muhimu ni kujenga ukuta,”.

Wakati wa kampeni ya kuchaguliwa kuwa rais, Trump aliahidi kuwa ikiwa atashinda, serikali yake itahakikisha kuwa inagharamia ukuta huo kwa kiasi cha Dola Bilioni 8.

Hata hivyo, serikali ya Mexico imesema haitagharamia ujenzi wa ukuta huo.