MAREKANI-MEXICO-USHIRIKIANO

Rais wa Mexico Enrique Peña Nieto afuta ziara yake mjini Washington

Rais wa Mexico Enrique Peña Nieto, hapa Januari 23, 2017 katika mji wa Mexico.
Rais wa Mexico Enrique Peña Nieto, hapa Januari 23, 2017 katika mji wa Mexico. REUTERS/Edgard Garrido

Siku moja baada ya kutiwa saini na Donald Trump amri kuanzisha ujenzi wa ukuta kwenye mpaka na Mexico, Rais wa Mexico Enrique Peña Nieto amesitisha Alhamisi hii, Januari 26 ziara yake ya mjini Washington, iliopangwa wiki ijayo.

Matangazo ya kibiashara

"Kama Mexico haiko tayari kugharamia ujenzi wa ukuta, ambao unahitajika, itakuwa bora kufuta mkutano ujao," Rais Donald Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter Jumatano wiki hii. Mwenzake wa Mexico amemjibu. Wakati ambapo alikua anapanga ziara ya kikazi mjini Washington wiki ijayo, Enrique Peña Nieto ametangaza Alhamisi ,pia kupitia Twitter, kwamba anafuta ziara yake ya mjini Washington. "Asubuhi hii nimeiarifu Ikulu ya White House kwamba sintohudhuria mkutano wa kikazi uliopangwa kufanyika Jumanne ijayo pamoja na rais wa Marekani," rais wa Mexico ameandika.

Donald Trump alifanya juhudi kubwa za kidiplomasia. Katika hotuba yake kwenye wizara ya usalama wa taifa Jumatano, Januari 25, rais wa Marekani alijizuia na uchokozi wowote ulioshuhudiwa wakati wa kampeni yake ya uchaguzi, amearifu mwandishi wetu mjini Washington, Anne-Marie Capomaccio. Alikuwa makini kwa kusema kwamba wananchi wa Mexico ni marafiki wa Marekani na kwamba ukuta inaotaka kujenga kwenye mpaka na Mexico ni jambo baya kwa nchi hizo mbili. Akiongeza kuwa kwa njia moja au nyingine, Mexico itagharamia ujenzi wa ukuta huo.

Lakini kukataa kwa rais wa Mexico kufadhili ujenzi wa ukuta huo kulisababisha rais Donald trump kupandwa na hasira. Chini ya wiki moja baada ya kuapishwa kwake, Rais wa Marekani anakabiliwa na tukio la kwanza la kidiplomasia.