MAREKANI

Mwanasheria mkuu wa Marekani ajiondoa kama sehemu ya uchungzi wa FBI kuhusu Urusi

Mwanasheria mkuu wa Marekani, Jeff Sessions.
Mwanasheria mkuu wa Marekani, Jeff Sessions. REUTERS/Yuri Gripas

Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Marekani, Jeff Sessions, amekubali shinikizo dhidi yake na kujiondoa kwenye jopo la uchunguzi wa shirika la upelelezi la FBI kuhusu nchi ya Urusi kuingilia uchaguzi wa mwaka jana.

Matangazo ya kibiashara

Mwanasheria huyo anasisitiza kuwa hakudanganya wakati alipohojiwa na kamati maalumu iliyoidhinisha uteuzi wake mwezi Januari mwaka huu, na kwamba hana chakusema kwa wakati huu kuhusu tuhuma dhidi yake.

Sessions anatuhumiwa kufanya mawasiliano na balozi wa Urusi wakati akiwa Seneta na hakuweka wazi wakati akihojiwa.

Uamuzi wake umekuja ikiwa ni siku chache tu zimepita toka kulipoibuliwa kwa tuhuma kuwa alidanganya hakuwi kufanya mawasiliano yoyote na viongozi wa Urusi, hali akijua fika kuwa aliwahi kuwasiliana na balozi wa Urusi.

Wabunge wa chama cha Democrats wanataka Sessions aachie ngazi nafasi yake kwa kile wanachohoji ni kwanini wakati akihojiwa na kamati ya bunge, hakusema chochote ikiwa aliwahi kufanya mazungumzo na maofisa wa Urusi.

Chama hicho kinataka Jeff Sessions achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kuidanganya kamati, wito ambao hata hivyo unapingwa na baadhi ya wabunge wa Republican.

Hivi karibuni aliyekuwa mshauri wa masuala ya usalama kwa rais Trump, Michael Flynn aliachia ngazi nafasi yake baada ya kubainika kuwa kabla ya uteuzi wake alifanya mawasiliano na balozi wa Urusi kuzungumzia vikwazo ilivyowekewa nchi hiyo.

Tayari shirika la upelelezi la FBI limeanza uchunguzi wa tuhuma kuwa Urusi iliingilia kwa sehemu kubwa uchaguzi wa nchi hiyo kwa lengo la kuhakikisha Donald Trump anakuwa rais.