MAREKANI

Majimbo zaidi Marekani yaenda mahakamani kupinga amri mpya ya Trump kwa wahamiaji

Majimbo kadhaa nchini Marekani yamesema yataenda mahakamani kupinga mpango mpya wa rais Donald Trump kuhusu wahamiaji ukilenga raia kutoka nchi sita za kiislamu pamoja na wakimbizi.

Rais wa Marekani, Donald Trump. Machi 2, 2017.
Rais wa Marekani, Donald Trump. Machi 2, 2017. REUTERS/Jonathan Ernst
Matangazo ya kibiashara

Jimbo la Washington, ambalo lilikuwa la kwanza kumshtaki Trump kutokana na amri yake ya awali iliyobatilishwa, limesema amri mpya aliyoitoa kuziba nafasi ya ile ya awali iliyokataliwa, inakiuka katiba kwa kuwabagua Waislamu.

Mwendesha mashtaka wa jimbo hilo, Bob Ferguson, amesema ombi lao la safari hii kwa mahakama ni kuomba zuio la mahakama kuhusu amri ya Trump.

"Ujumbe wangu kwa rais Trump ni huu, usiwe na haraka sana," alisema Ferguson. "Baada ya kutumia miezi kadhaa kukarabati amri ya awali aliyokurupuka, amri mpya ya rais inazo baadhi ya sheria zilezile zilizokuwepo kwenye amri ya awali."

Waandamanaji wakiwa na mabango yanayokashifu amri mpya ya rais Donald Trump kuhusu wahamiaji
Waandamanaji wakiwa na mabango yanayokashifu amri mpya ya rais Donald Trump kuhusu wahamiaji REUTERS/Eric Thayer

Wanasheria kwenye majimbo ya New York, Massachusetts na Oregon, wamesema wamechukua hatua kama ya jimbo la Washington sambamba na jimbo la Minnesota kupinga amri hii ya mahakama.

Upinzani wa majimbol haya umekuja baada ya jimbo la Hawaii kuwasilisha pingamizi mahakamani kupinga agizo jipya la Trump.

Agizo jipya la Trump alilolitia saini Jumatatuj ya wiki hii, linakataza kutolewa kwa visa mpya kwa raia kutoka nchini Syria, Iran, Somalia, Libya, Sudan na Yemen huku kwa muda ikisitisha mpango wa wakimbizi kwa siku 120.

Agizo hili jipya linatarajiwa kuanza kazi Machi 16 mwaka huu lakini halitawahusu wasafiri ambao tayari wako ndani ya Marekani na wana viza.