MAREKANI-TRUMP

Rais Trump matatani tena nyaraka zake za ulipaji kodi zavuja

Rais wa Marekani, Donald Trump.
Rais wa Marekani, Donald Trump. © REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump alilipa kiasi cha dola milioni 38 kama tozo ya kodi mwaka 2005, huku ikulu ya Washington ikikiri kuwa nyaraka zilizovuja ni za kweli na kutoa maelezo ya kina kuhusu kodi aliyolipa kiongozi huyo.

Matangazo ya kibiashara

Nyaraka hizi za siri zinazoonesha kiasi cha kodi alicholipa Donald Trump, zilichapishwa na kuoneshwa kwenye vyombp vingi vya habari nchini Marekani.

Rais Trump amekataa kuweka hadharani nyaraka zake za ulipaji kodi na mapato anayoyapata kutokana na biashara zake, jambo ambalo limevunja utamaduni wa karibu miaka 40 kwa wanasiasa kuweka wazi mapato na kodi walizolipa kwa Serikali.

Taarifa hii iliyovuja, ni sehemu tu ya malipo ya kodi aliyoyafanya kwa mwaka mmoja kutoka kwenye nyaraka za karibu mwongo mmoja uliopita, huku nyaraka yenyewe ikionesha kukanganya.

Ikulu ya White House, imethibitisha taarifa zilizochapishwa punde tu baada ya kuwekwa wazi na mwandishi wa habari za uchunguzi, David Cay Johnston, ikulu hiyo ikisema itatoa taarifa zaidi.

Nyaraka hii hata hivyo imeonekena kumuunga mkono Trump, ambaye toka awali amekuwa akisisitiza kuwa amelipa kodi zake sawa na anavyotakiwa kisheria.

Hata hivyo nyaraka hii ya mwaka 2005 inaonesha tu kiasi anachodai, lakini haikuonesha kabisa vyanzo vya mapato yake, suala ambalo huenda likajibu masuali kuhusu utata wa biashara zinazofanywa na Trump.

Nyaraka hiyo inaonesha kuwa Trump na mke wake Melania, wanalipa kiasi cha dola milioni 5.3 kama wanavyotakiwa na Serikali kuu, kiasi ambacho ni pungufu ya asilimia nne, amesema mwandishi aliyevujisha nyaraka hiyo.

Mfumo wa AMT uliotumiwa na Trump ulianzishwa kwa lengo la kuwadhibiti watu matajiri na wafanyabiashara wakubwa kutotumia mwanya kukwepa kodi, hivyo hii ni kodi ya ziada wanayolipa, sheria ambayo hata hivyo Trump anataka ibatilishwe.

Johnstone hata hivyo akihojiwa na kituo cha televisheni cha MSNBC, amesema hafahamu mtu aliyevujisha nyaraka hiyo.