MAREKANI-FBI-URUSI-UCHUNGUZI

James Comey: FBI inachunguza madai kuwa Urusi iliingilia uchaguzi Marekani

Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani FBI James Comey, Machi 20, 2017.
Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani FBI James Comey, Machi 20, 2017. REUTERS/Joshua Roberts

Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani FBI James Comey, amesema kuwa FBI inaendesha uchunguzi wa madai kuwa Urusi iliingilia kati Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016.

Matangazo ya kibiashara

Uchunguzi huu unahusu kuwepo uwezekano wa uhusiano kati ya watu kwenye kampeni ya Trump na serikali ya Urusi, na ikiwa kulikuwa ushirkiano kati ya kampeni ya Trump na Urusi.

Mkurugenzi huyo wa FBI alikuwa akizungumza katika kikao kisicho cha kawaida cha kamati ya bunge la Congress, ambayo pia inachunguza uwezekano wa kuwepo ushirikiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi.

Bwana Comey amebaini kwamba uchunguzi wanaofanya ni mgumu na kuongeza kuwa hawezi kuipa kamati hiyo taarifa za kina ambazo bado hazijatolewa kwa umma.

Uamuzi huo wa FBI unakuja wakati ambapo Rais Donald Trump ameendelea kukana kuhusika kwa njia yoyote ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani. Hata hivyo Urusi mara nyingi imekana majaribio ya kushawishi uchaguzi wa Marekani.