MAREKANI

Rais Trump apata pigo baada ya wabunge kukataa mswada wake wa bima ya afya

Donald Trump  baada ya kupoteza uungwaji mkono wa kubadilisha bima ya afya ya  Obamacare.
Donald Trump baada ya kupoteza uungwaji mkono wa kubadilisha bima ya afya ya Obamacare. REUTERS/Carlos Barria

Rais wa Marekani Donald Trump ameondoa mswada wake wa Bima ya afya baada ya kutopata uungwaji mkono hasa kutoka kwa wabunge wa Congress.

Matangazo ya kibiashara

Spika wa bunge hilo Paul Ryan amewaambia wabunge kuwa Trump amelazimika kuondoa mswada baada ya kuonekana wazi kuwa umeshindwa kupata uungwaji mkono wa wabunge 215.

Hili ni pigo kubwa kwa rais Trump na uamuzi wa Congress unamaanisha kuwa, mpango wa bima ya afya wa rais wa zamani Barrack Obama, Obamacare utaendelea kutumiwa nchini humo.

Trump wakati wa kampeni zake mwaka uliopita, alikuwa ameahidi kubadilisha  bima ya Obamacare na kuleta bima nyingine.

Kabla ya kushindwa kwa mswada huo, Trump aliwaambia wabunge wa Republican kuwa ikiwa wasingeupitisha mswada huo, nchi hiyo ingebaki na mpango wa Obamacare.

Wabunge wengi wa chama cha Republican waliupinga mswada huo baada ya kuonekana kuwa ni ghali sana na hivyo kuhatarisha uwezekano wa  Wamarekani wa kipato cha chini na kati kukosa kupata bima hiyo.