MAREKANI

Ivanka Trump kumshauri baba yake katika Ikulu ya Marekani

Ivanka Trump bintiye Donald Trump
Ivanka Trump bintiye Donald Trump REUTERS/Jim Bourg

Ikulu ya Marekani imetangaza kuwa Ivanka Trump, bintiye rais Donald Trump atakuwa msaidizi wa baba yake.

Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo, Ivanka hatalipwa mshahara wowote katika ajira hii mpya ya kumsaidia na kumshauri baba yake.

Ivanka mwenye umri wa miaka 35 amesema baada ya mjadala mrefu yeye binafasi ameamua kwenda kumshauri baba yake bila malipo ili kuondoa upendeleo wowote.

Anaungana na mume wake Jared Kushner ambaye ni mshauri Mkuu wa rais Trump.

Wiki iliyiopita, kulikuwa na ripoti kuwa Ivanka angepewa kazi hiyo bila kufuata utaratibu wa Ikulu na wa utumishi wa umma hali ambayo ilizua ukosoaji mkubwa kutoka wakosoaji wa rais Trump na kuuita upendeleo wa kifamilia.

Hata hivyo wakili wa Ivanka Jamie Gorelick, amesema taratibu zote zimefuatwa ili kuweka kila kitu wazi na kuepuka kuwepo kwa mashaka yoyote.

Nafasi hii itampa Ivanka fursa ya kufahamu siri za serikali za Ikulu ya Marekani na kumshauri baba yake.
Hii ndio mara ya kwanza kwa Ivanka na mumewe kufanya kazi katika Ofisi za umma.