AFGHANISTAN-IS-MAREKANI

Aghanistan: Bomu kubwa zaidi kuwahi kutumiwa na Marekani laua mamia ya wapiganaji wa IS

Bomu aina ya MOAB lenye uzito wa tani 11 ambalo kwa mara ya kwanza limetumiwa na Marekani nchini Afghanistan.
Bomu aina ya MOAB lenye uzito wa tani 11 ambalo kwa mara ya kwanza limetumiwa na Marekani nchini Afghanistan. Elgin Air Force Base/Handout via REUTERS

Bomu kubwa zaidi kuwahi kutengenezwa na Marekani na ambalo halitumii nyuklia limeangushwa kwenye milima ya Afghanistan na kuripotiwa kuwaua mamia ya wapiganaji wa kundi la Islamic State ambao wamekuwa wakijificha kwenye mahandaki.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Afghanistan imethibitisha kudondoshwa kwa bomu hilo, ambalo pamoja na nguvu kubwa ya uharibifu inayotokana na silaha hiyo, mamlaka nchini humo zimekanusha taarifa kuwa kuna raia wa kawaida waliouawa.

Bomu hilo aina ya GBU-43/B Massive Ordnance Air Blast, linafahamika kwa jina jingine kama “Mama wa mabomu yote” na limetumiwa kwa mara ya kwanza kulenga ngome za wapiganaji wa IS mashariki mwa jimbo la Nangarhar hapo jana jioni.

Bomu hili lilitarajiwa kumaliza kabisa uwezo wa kundi la Islamic State nchini Afghanistan na kutuma onyo kwa kundi la Taliban ambalo linajiandaa na mashambulizi yake ya mwaka.

“Matokeo ya bomu hilo, yamesaidia kusambaratisha maficho ya IS na wapiganaji wake 36 kuuawa,” imesema taarifa ya wizara ya manbo ya ndani ya Afghanistan, ikisema shambulizi la bomu hilo limetekelezwa kwa ushirikiano na vyombo vya usalama kwenye mji huo.

Bomu hili lilirushwa kwa kutumia ndege maalumu ya kijeshi aina MC-130 na lilikuwa na uzito wa tani 11, na limetenegenezwa maalumu kwaajili ya kufanya mashambulizi ya kusambaratisha kabisa ngome za wapiganaji na kwa eneo kubwa zaidi.

Mlipuko wa bomu hilo ulisikika kwenye umbali mkubwa wa jimbo la Nangarhar na kusambaza moto kuharibu kile ambacho maofisa wa Afghanistan wanasema mtandao wa kundi la IS waliokuwa wakitumia mashimo kujificha.

Shambulizi hili limetekelezwa wakati huu kukiwa na vita kubwa dhidi ya makundi ya kiislamu huku Serikali ya Marekani ikizidisha mashambulizi dhidi ya wapiganaji hao.

Limekuja pia ikiwa ni juma moja tu limepita baada ya rais Donald Trump kuagiza kutekelezwa kwa mashambulizi kwenye uwanja wa jeshi la Syria kwa kile ilichodai kuwa utawala wa rais Assad kutekeleza shambulio la silaha za kemikali.

Rais Trump amesifu shambulio hili ambalo amesema limekuwa la mafaniko sana.