MAREKANI-KOREA KASKAZINI-USALAMA

Donald Trump kukutana na Maseneta kuhusu Korea Kaskazini

Maseneta wa Marekani waalikwa kuhudhuria kikao kuhusu Korea Kaskazini katika Ikulu ya White House
Maseneta wa Marekani waalikwa kuhudhuria kikao kuhusu Korea Kaskazini katika Ikulu ya White House PHOTO MARK WILSON / GETTY IMAGES NORTH AMERICA / AFP

Bunge lote la Seneti nchini Marekani limealikwa kwa kikao cha kupashwa habari kuhusu Korea Kaskazini siku ya Jumatano katika ikulu ya White House. Hili ni tukio ambalo si la kawaida.

Matangazo ya kibiashara

Ikulu ya White House amewaalika maseneta 100 wa Marekani kuhudhuria mkutano kuhusu Korea Kaskazini Jumatano hii 26 Aprili. Maudhui ya mkutano huu usio wa kawaida, hayatowekwa wazi kwani siri. Mawaziri husika watawafahamiha Maseneta hao taarifa za hivi karibuni kuhusu swala hilo.

Kikao hiki kinakuja wakati ambapo Korea Kaskazini, siku ya Jumatatu, ilifanya zoezi kubwa la kijeshi ambapo ufyatuaji wa risasi ulifanyika ili kuadhimisha miaka 85 tangu uzinduzi wa jeshi lake.

Wasiwasi umeendelea kuongezeka kuhusu uwezekano wa Korea Kaskazini kufanya jaribio jingine la kombora au silaha za nyuklia.

Mapema siku ya Jumatatu jioni Mamlaka ya Korea Kusini ilisema kuwa idadi kubwa ya vifaa vyake vya kijeshi vimepelekwa katika eneo la Wonsan kwa zoezi la kijeshi.

Korea Kusini pia ilisema kuwa wanamaji wake wamekuwa wakifanya mazoezi ya pamoja na meli za kijeshi za Marekani.

Hayo yanajiri wakati ambapo nyambizi ya jeshi la Marekani iliwawasili katika pwani ya Korea Kusini toka siku ya Jumatatu.

Meli hiyo inatarajiwa kushiriki kwenye mazoezi ya kijeshi pamoja na kundi la meli zinazoongozwa na Carl Vinson, kundi ambalo lilitumwa eneo la Korea kuonyesha ubabe wa kijeshi wa Marekani.

Hata hivyo Korea Kaskazini ilisema hivi karibuni kuwa itajibu shambulizi lolote la Marekani katika ardhi yake.