VENEZUELA-MAANDAMANO-USALAMA

Rais wa Venezuela akosolewa kuhusu mpango wa kuunda bunge jipya

Wafuasi waendelea na maandamano yao mjini Caracas, Venezuela.
Wafuasi waendelea na maandamano yao mjini Caracas, Venezuela. REUTERS/Marco Bello

Wakati ambapo maandamano yanaendelea kushika kasi katika mitaa mbalimbali ya miji tofauti ya Venezuela, viongozi mbalimbli wameanza kumkosoa Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kuhusu mpango wake wa kuunda bunge litakaloandika katiba mpya.

Matangazo ya kibiashara

Marekani imesema kuwa bunge la katiba ni njama za kumfanya Maduro aendelee kusalia madarakani. Brazil kwa upande wake imesema kuwa huo ni mpango wa kufanya mapinduzi.

Katibu mkuu wa jumuia ya nchi za Amerika, OAS, Luiz Almagro amesema hatua hiyo haikubaliki na ni kinyume cha katiba.

Bunge la Congress linalodhibitiwa na upinzani limepiga kura kukataa bunge jipya la katiba, likisema kuwa halitaundwa bila wao kuridhia.

Kiongozi wa upinzani Henrique Capriles amekosoa kauli ya rais Nicolas Maduro kwa kuwashtumu wapinzani kwamba wao ndio walitaka kumpindua.

Henrique Capriles amesema hayo ni maneno ya serikali iliyoshindwa ambayo inataka kukwepa kuitisha uchaguzi.