MAREKANI

Republicans wapiga kura ya ndio kufuta bima ya afya ya Obamacare

Rais wa Marekani Donald Trump  akiwa na wabunge wa Republican katika Ikulu ya White House baada ya kupitishwa kwa mswada wa kutupilia mbali bima ya afya ya Obamacare
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa na wabunge wa Republican katika Ikulu ya White House baada ya kupitishwa kwa mswada wa kutupilia mbali bima ya afya ya Obamacare REUTERS/Carlos Barria

Wabunge wa chama cha Republican nchini Marekani wamefanikiwa kupitisha mswada unaondoa na kubadilisha mpango wa  bima ya afya ya Obamacare iliyoanzishwa na rais wa zamani Barrack Obama.

Matangazo ya kibiashara

Mswada huo ulipita baada ya wabunge wa Republican kufanikiwa kupata kura 217 dhidi ya 213, hatua ambayo inaonekana ni ushindi kwa rais Donald Trump ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipinga bima hii.

Trump aliyekutana na viongozi wa Republican katika IKulu ya White House, amesema amefurahia sana mafanikio ya wabunge wake na kusisitiza kuwa bima ya Obamacare imekufa.

Kulikuwa na maandamano nje ya majengo ya bunge jijini Washington DC kupinga hatua ya wabunge wa Republican. Hakuna mbunge yeyote wa Democratic aliyeunga mkono mswada huo ambao sasa utapigiwa kura katika bunge la Senate.

Wanaisasa wa Democratic akiweno Hillary Clinton aliyewania urais mwaka uliopita, wamelaani hatua hiyo na kusema inaondoa matumaini ya Wamarekani wa kipato cha chini kupata haki ya kupata huduma ya afya.

Serikali ya Trump inatarajiwa kutumia Dola za Marekani Milioni 8, kuzindua mpango mpya wa bima ya afya, mpango ambao hata hivyo unakosolewa sana na watalaam wa afya na wanasiasa wa upinzani kuwa utawaacha raia wengi bila bima.