MAREKANI

Trump ajikanganya mwenyewe kuhusu kumfuta kazi mkurugenzi wa FBI

Rais wa Marekani Donald Trump na aliyekuwa mkurugenzi wa FB James Comey.
Rais wa Marekani Donald Trump na aliyekuwa mkurugenzi wa FB James Comey. REUTERS/Jim Lo Scalzo/Pool, Gary Cameron/File Photo

Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwa muda mrefu toka aingie madarakabi amekuwa akitaka kumfuta kazi aliyekuwa mkurugenzi wa shirika la upelelezi la nchi hiyo FBI, James Comey, akikinzana na matamshi yake ya awali kuwa alichukua uamuzi huo baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa mwanasheria mkuu wa Serikali.

Matangazo ya kibiashara

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha NBC, rais Trump amesema alikuwa amfute kazi Comey licha ya mapendekezo aliyopewa na mwanasheria mkuu wa Serikali, hatua ambayo hata ikulu ya Washington imeshindwa kulishawishi bunge la Congress na wananchi.

Trump amesisitiza ulikuwa ni uamuzi wake binafsi kumfuta kazi Comey akimkosoa namna ambavyo amekuwa akifanya shughuli zake huku kwa mara ya kwanza akiweka wazi kuwa alimuuliza mkurugenzi huyo kwa zaidi ya mara tatu ikiwa uchunguzi unaoendelea una muhusu.

Matamshi haya ya Trump tayari yamezua mjadala kuhusu kiongozi huyo kutumia madaraka yake vibaya kwa kuingilia uchunguzi wa mihimili huru, huku wabunge wa Democrats wakisema ni muendelezo wa Trump kuwadharau wanaume na wanawake wanaohudumu kwenye vyombo vya usalama vya nchi hiyo.

Rais Trump ameongeza kuwa wakati akichukua uamuzi huo nchi ya Urusi ilikuwa kwenye mawazo yake ambapo hapo jana pia alikutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov.