MAREKANI-KOREA KASKAZINI

Trump apendekeza vikwazo zaidi dhidi ya Korea Kaskazini baada ya kufanya jaribio jingine

Rais wa Marekani Donald Trump.
Rais wa Marekani Donald Trump. REUTERS/Carlos Barria

Rais wa Marekani Donald Trump ametaka kutangazwa vikwazo vigumu zaidi kwa nchi ya Korea Kaskazini baada ya nchi hiyo kufanya jaribio jingine la kombora la masafa marefu, jaribio linaloonekana kama ni kuupima utawala mpya wa Korea Kusini ambao hauna msimamo mkali dhidi yake.

Matangazo ya kibiashara

“Hebu jaribio hili lituamshe kama mataifa ili tuchukue hatua kali zaidi za vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini,” imesema taarifa iliyotolewa na ikulu ya White House.

Kombora hilo limeripotiwa kusafiri umbali wa kilometa 700 kabla ya kuangukia kwenye pwani ya bahari ya Japan upande wa mashariki.

Lililipuka jirani kabisa na ardhi ya Urusi… sidhani kama rais wake anafikiri Urusi imependa kitendo kile, imeongeza taarifa ya ikulu ya Marekani iliyosema Korea Kaskazini imeendelea kuleta dharau kwa dunia.

Hata hivyo baada wizara ya mambo ya ndani ya Urusi ilitoa taarifa ikisema kuwa kombora hilo lilianguka kwenye umbali wa kilometa 500 kwenye mpaka wa nchi yake lakini halikuwa na madhara yoyote.

Mshauri wa masuala ya usalama wa Marekani H.R. McMaster amewasiliana kwa njia ya simu na wenzake wa Korea Kusini na Japan kuhusiana na jaribio hili.

Nchi ya China ambayo imekuwa kwenye shinikizo kubwa kutoka kwa Marekani kuhusu kuchukua hatua dhidi ya Korea Kaskazini, imetaka pande hizo kujiepusha na vitendo vinavyochochea uhasama.

Vikwazo kadhaa vya umoja wa Mataifa na Marekani vilivyowekwa dhidi ya Korea Kaskazini vimekuwa na athari kidogo kwa Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa kuendeleza vinu vya nyuklia.

Kabla ya jaribio hili Marekani ilisema inaangalia namna zote za kuhakikisha inakata misaada yote ya kifedha dhidi ya Korea Kaskazini.

Rais Trump ametishia kuishambulia kijeshi nchi ya Korea Kaskazini lakini hivi karibuni ikalegeza msimamo wake ikisema iko tayari kukutana na kiongozi wa taifa hilo Kim Jong-Un.