VENEZUELA-MAANDAMANO-USALAMA

Raia waendelea kuandamana Venezuela

Upinzani wazuia barabara kuu nchini Venezuela, Jumatatu Mei 15, 2017, Caracas.
Upinzani wazuia barabara kuu nchini Venezuela, Jumatatu Mei 15, 2017, Caracas. REUTERS/Christian Veron

Hali ya sintofahamu imeendelea kushuhudia katika miji mbalimbali nchini Venezuela kufuatia maandamano yanayoendelea nchini humo. Kijana mdogo mwenye umri wa miaka 17 ameuawa katika siku nyingine ya maandamano dhidi ya rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro.

Matangazo ya kibiashara

Watu kadhaa wamekamatwa na wengine hawajulikani walipo, kwa mujibu wa mashirika ya kiraia nchini Venezuela. Kwa sasa maandamano yanazorotesha uchumi wa taifa hilo.

Upinzani unasema kwamba zaidi ya watu 40 walikamatwa siku ya Jumatatu katika jimbo la Tachira.

Luis Alviarez alipigwa risasi kifuani katika maandamano yaliyoitishwa na upinzani kwenye mji wa Guasimo, Mashariki mwa Venezuela.

Kiongozi wa wanafunzi mwenye umri wa miaka 22 Wilmer Arevalo yukomahututi baada ya kupigwa risasi kichwani kwenye maandamano mengine.

Tayari wito umetolewa wa kufanyika kwa uchunguzi kuhusu mazingira ya mauaji hayo.

Takriban watu 40 wameuawa tangu maandamano kuanza nchini humo majuma saba yaliyopita.