Trump asema Marekani na Israel hazitakubali Iran kutengeneza silaha za Nyuklia
Imechapishwa: Imehaririwa:
Rais wa Marekani Donald Trump anayezuru Israeli, amesema Iran isiruhusiwe kutengeneza silaha za Nyuklia.
Akizungumza mjini Jerusalam, rais Trump ameishtumu Tehran pia kwa kuyasaidia makundi ya kigaidi kama Islamic State katika eneo ya Mashariki ya Kati.
“Iran isikubaliwe kutengeza na kuwa na silaha za nyuklia,” alisema Trump baada ya kukutana na rais Reuven Rivlin.
Awali akizungumza akiwa mjini Tel Aviv baada ya kuwasili nchini humo, kiongozi huyo alisisitiza kuwa Marekani itaendelea kushirikiana na Israel katika maswala mbalimbali hasa ya kiusalama.
Aidha, ameelezea umuhimu wa kufufua mazungumzo ya amani kati ya Israeli na Palestina.
“Ziara yangu ya kwanza nje ya nchi, nimekuja katika eneo hilo takatifu kuthibitisha uhusiano wetu wa Israel na Marekani,” amesema Trump.
“Tuna nafasi ya kipekee ya kuleta amani , usalama na udhabiti katika eneo hili na watu wake, lakini zaidi ya yote kushinda ugaidi,” aliongeza.
Siku ya Jumanne atakutana na kiongozi wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas.
Trump ambaye ametokea nchini Saudi Arabia, anatarajiwa pia kuzuru Vatican kuonana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis.