MAREKANI-ISRAEL

Trump asema atafanya awezalo kusaidia kuleta amani kati ya Israel na Palestina

Rais Donald Trump (Kushoto) alipokutana na rais wa Palestina Mahmud Abbas (Kulia) Mei  23 2017
Rais Donald Trump (Kushoto) alipokutana na rais wa Palestina Mahmud Abbas (Kulia) Mei 23 2017 Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump amesema atafanya kila kilicho ndani ya uwezo wake kufufua na kufanikisha mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Matangazo ya kibiashara

Kauli ya Trump imekuja baada ya kukutana na kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas mjini Bethlehem katika eneo la ukingo wa Magharibi.

Israel na Palestina hazijawa na mazungumzo ya moja kwa moja ya kusaka amani kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Trump amekiri kuwa kufanikisha mazungumzo hayo ni kazi kubwa na ngumu.

Hata hivyo, amesema hatua ya kwenda mjini Bethlehem na kukutana na rais Abbas ni ishara ya tumaini la kuleta tumaini la mwafaka.

“Ninajaribu kuleta amani kati ya Wapalestina na Waisraeli na nitajitahidi kwa uwezo wangu wote kufanikisha hilo,” alisema rais Trump.

Baada ya kukutana na rais Abbas, Trump ambaye anamalizia ziara yake katika eneo la Mashariki ya Kati hivi leo, alirejea mjini Jerusalem na kukutana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Trump amesema uhusiano kati ya Marekani na Israeli hauwezi kuvunjika na mataifa hayo mawili yataendelea kushirikiana katika maswala ya usalama na kushinda ugaidi.

"Serikali yangu siku zote itasimama na Israel," rais Trump aliwaambia Waisraeli.

Baada ya kuondoka Israel, Trump anakwenda nchini Italia kukutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis mjini Vatican.

Siku ya Ijumaa na Jumamosi, atahudhuria mkutano wa nchi zenye utajiri wa viwanda wa G 7 siku ya Ijumaa na Jumamosi mjini Taormina nchini Italia.