MAREKANI-WAHAMIAJI

Rais Trump ataka Mahakama ya Juu kukubali agizo lake kuhusu wahamiaji

Rais wa Marekeani Donald Trump
Rais wa Marekeani Donald Trump © REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump ameitaka Mahakama ya Juu kusikiliza kwa haraka rufaa iliyowasilishwa kupinga agizo lake la kuwazuia raia kutoka Mataifa sita ya Kiislamu kuzuru nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump amesema Wizara ya Haki iliyowasilisha rufaa hiyo inastahili kutetea uamuzi huo ili Mahakama itoe agizo la kuunga mkono hatua yake.

Aidha, amesema kuwa Marekani inawafanyia uchunguzi wa kina wageni wote wanaoingia nchini humo kwa sababu za kiusalama.

“Tunawafanyia msako mkali wale wote wanaokuja nchini Marekani, hii itasaidia sana kuiwekea nchi yetu salama,”

“Mahakama zinafanya kazi zake polepole na zinatumiwa kisiasa,” aliandika rais Trump kupitia ukursa wake wa Twitter.

Wanaharakati wa kutetea haki za Binadamu miezi kadhaa iliyopita walikwenda Mahakamani, na kufanikiwa kupata agizo la Mahakama kuzuia kutekelezwa kwa uamuzi wa rais Trump.

Raia kutoka Iran, Libya, Somalia, Sudan, Syria na Yemen walikuwa wameanza kuathirika na uamuzi wa Trump lakini walipata afueni baada ya kuwasilishwa kwa kesi Mahakamani.

Mahakama iliamua kusitisha agizo la Trump muda kwa kile walichokisema ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu.

Trump wakati akifanye kampeni za Uchaguzi mwaka uliopita, aliahidi kutowaruhusu Waislamu kuja nchini humo kwa sababu za kiusalama.