MAREKANI-ULINZI

Donald Trump kupiga marufuku wanaobadili jinsia kuhudumu katika jeshi

Rais Donald Trump amesema Marekani haitaruhusu ama kukubali watu wanaobadili jinsia kuhudumu katika kiwango chochote cha jeshi nchini Marekani.
Rais Donald Trump amesema Marekani haitaruhusu ama kukubali watu wanaobadili jinsia kuhudumu katika kiwango chochote cha jeshi nchini Marekani. REUTERS/Yuri Gripas

Donald Trumpamewashangaza wengi, ikiwa ni pamoja na Pentagon, akitangaza siku ya Jumatano, Julai 26 katika mfululizo wa taarifa kadhaa kwenye ukurasa wake wa Twitter marufuku kwa watu wanaobadili jinsia kuhudumu katika jeshi la Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Rais Donald Trump alisema watu wanaobadilisha jinsia zao wataligharimu jeshi kimatibabu na kuvuruga maisha ya kawaida jeshini.

Hadi sasa, askari ambao walibadili jinsia zao wakiwa katika jeshi hawatofukuzwa kazini. Utawala wa Barack Obama ulikubali ajira ya watu wanaobadili jinsia zao, ajira ambayo ingelianza mwaka huu.

Uamuzi huo wa Donald Trump haukushangaza wizara ya ulinzi, ambayo haikua na taarifa kuhusu uamuzi huo, lakini pia ulizua hali ya sintofahamu kutoka pande zote katika wigo wa kisiasa.

Mapema mwezi huu waziri wa Ulinzi wa Marekani, James Mattis, alisimamisha uajiri wa watu wanaobadilisha jinsia zao kwa miezi sita.

Kwa mujibu wa shirika la Independent Rand Corporation, mnamo mwaka 2016 wanajeshi 2,450 kati ya wanajeshi milioni 1.2 ni watu waliobadili jinsia. Hata hivyo wanaharakati wanasema kuwa idadi hiyo huenda ikawa juu.

Katika msururu wa ujumbe wa Twitter bwana Trump alisema “baada ya majadiliano na majenerali pamoja na wataalam wa kijeshi tafadhali nawashauri kwamba Marekani haitaruhusu ama kukubali watu wanaobadili jinsia kuhudumu katika kiwango chochote cha jeshi nchini Marekani.”

Jeshi linafaa kuwa na lengo moja la kuibuka mshindi na haliwezi kugubikwa na mzigo wa gharama ya juu ya matibabu ambayo watu wanaotaka kubadili jinsia wangehusishwa nayo, “ aliongeza rais Trump.

Marufuku hiyo kwa wapenzi wa jinsia moja wanaojulikana kama ''don't Ask don't tell'' iliondolewa 2011.