MAEAKNI-TRUMP-TABIA NCHI

Trump kuzuru Puerto Rico baada ya kuathiriwa na kimbunga Maria

Kisiwa cha Puerto Rico kinachomilikiwa na Marekani, ambacho kiliathiriwa vibaya na kimbunga Maria.
Kisiwa cha Puerto Rico kinachomilikiwa na Marekani, ambacho kiliathiriwa vibaya na kimbunga Maria. Ricardo ARDUENGO / AFP

Rais wa Marekani Donald Trump alisema siku ya Jumanne kwamba anapanga kuzuru Puerto Rico wiki ijayo ili kufuta shutma kuhusu kujikokota kwa misaada iliyotolewa na utawala wake kwenye eneo hilo linalomilikiwa na Marekani lililoharibiwa na kimbunga Maria.

Matangazo ya kibiashara

Rais Trump alikutana na Ricardo Rossello, gavana wa Puerto Rico, siku ya Jumanne na akamuahidi kuwa "msaada utaendelea kutolewa" kutoka serikali ya shirikisho.

Bw. Trump alistumiwa kuwapuuzia wakazi milioni 3.4 wa kisiwa hiki kama raia wa eneo la pili, wakati ambapo wakazi wa Puerto Rico wana urai wa Marekani, hata kama hawana haki ya kupiga kura. Kwa mujibu wa wakosoaji wake, misaada ya serikali ya Marekani iliharakishwa katika majimbo ya Texas na Florida, yaliyoathirika wakati huo na vimbunga Harvey na Irma mwishoni mwa mwezi Agosti na mapema mwezi Septemba mwaka huu.

Wiki moja baada ya kupita kwa kimbunga Maria, misaada inawasili kwa kiwango kidogo katika kisiwa cha Puerto Rico, ambacho kinakabiliwa na ukosefu wa maji ya kunywa, umeme au mafuta. Shughuli za kusafisha pia zinajikokota kuanza.

"Ni vigumu sana, kwa sababu kila kitu kinapimwa. Hata kuwa na mfuko wa mchele ni vigumu," mkazi wa Bayamon (kaskazini mashariki mwa Puerto Rico) ameliambia shirika la habari la AFP.

Kwa mujibu wa mamlaka, watu 11,437 walikuwa bado wamehifadhiwa katika majengo ya serikali. Tangu siku ya Jumatatu jioni, malori 150 yaliyojaa mafuta yalisambaza mafuta hayo kwenye vituo mbalimbali vya mafuta. Asilimia 42 ya wa kazi wa kisiwa hicho hawana maji ya kunywa na hospitali 21 tu kwa jumla ya 69 ndizo zinahudumu.