MAREKANi-USALAMA

Watu 26 wauawa kwa kupigwa risasi kanisani Texas, Marekani

Janga hilo lililotokea katika kanisa hili katika eneo la Sutherland Springs, kilomita 60 hivi mashariki mwa mji wa San Antonio, kusini magharibi mwa Texas Novemba 5, 2017.
Janga hilo lililotokea katika kanisa hili katika eneo la Sutherland Springs, kilomita 60 hivi mashariki mwa mji wa San Antonio, kusini magharibi mwa Texas Novemba 5, 2017. MAX MASSEY/ KSAT 12/via REUTERS

Mtu mwenye kujihami kwa bunduki aliwaua kwa kuwapiga risasi watu 26 wakati wa ibada katika kanisa la Sutherland Springs, katika jimbo la Texas, nchini Marekani. Tukio hilo lilitokea siku ya Jumapili Novemba 5.

Matangazo ya kibiashara

Watu ishirini walijeruhiwa. Gavana wa Texas, Greg Abbott, ametaja kitendo hicho kuwa ni cha ukatili. Mshambuliaji pia alifariki baada ya kupigwa risasi na mkazi mmoja wa eneo hilo alipokua akijaribu kutoroka.

Afisa mkuu wa idara ya usalama wa Texas Freeman Martin amesema watu wote waliouawa walikuwa na umri wa kati ya miaka 5 na 72.

Kwa mujibu wa maafisa wa usalama wa Marekani mshukiwa ni mwanamume mzungu wa umri wa miaka 20 ambaye alikuwa amevalia mavazi meusi na fulana ya kujikinga dhidi ya risasi pamoja na kuwa na bunduki yenye uwezo mkubwa.

Mshambuliaji alikuta amefariki ndani ya gari lake, baada ya kupigwa risasi na mkazi mmoja wa eneo la Sutherland Springs, eneo lenye wakazi 400 lililo karibu na San Antonio.

Mshukiwa ametajwa kuwa Devin P Kelley, 26, kwa mujibu wa vyombo vya jhabari Marekani. Laiki polisi bado hawajathibitisha jina lake.

Rais wa Marekani, Donald trump, ambaye anazuru Japan, amehutubia raia wa Marekani baada ya tukio hilo, akimtaka Gavana wa Texas kuanza mkutano wake na waandishi wa habari akilani "mauaji" haya ya kutisha. Kabla ya hapo, alikuwa ametuma ujumbe kwenye ukurasa wake wa Twitter kwa wakazi wa eneo hilo lililokumbwa na mkasa huo akisema: "Naomba Mungu awasaidie wakazi wa Sutherland Springs." Ameongeza kuwa "anafuata hali hiyo kwa karibu kutoka Japan" ambako yuko ziarani.