MAREKANI-TRUMP-HAKI

Mashtaka mapya yaibuka dhidi ya mgombea wa chama cha Republican

Beverly Young Nelson anamshtumu mgombea wa uchaguzi mdogo wa Seneti  kwa tiketi ya chama cha Republican, Roy Moore, kumdhalilisha kingono, katika mkutano na waandishi wa habari New York tarehe 13 Novemba 2017.
Beverly Young Nelson anamshtumu mgombea wa uchaguzi mdogo wa Seneti kwa tiketi ya chama cha Republican, Roy Moore, kumdhalilisha kingono, katika mkutano na waandishi wa habari New York tarehe 13 Novemba 2017. AFP

Mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi mdogo wa seneti wa Desemba 12 katika jimbo la Alabama, Roy Moore anaendelea kukabiliwa na mashtaka mbalimbali ya unyanyasaji wa kijinsia.

Matangazo ya kibiashara

Mwanamke mwengine amemshtumu siku ya Jumatatu kumfanyia unyanyasaji wa kijinsia, wakati ambapo kambi yake imeendelea kumtaka ajiondoe kwenye kinyang'anyiro hicho.

Siku ya Alhamisi juma lililopita gazeti la Washington Post lilichapisha habari ya mwanamke anayedai kuwa alidhalilishwa kingono nyumbani kwa Roy Moore mwaka 1979 akiwa na umri wa miaka 14.

Gazeti la kila siku la Capital pia lilichapisha habari ya wanawake wengine watatu, ambao kila mmoja alidai kuwa aliitishwa kwa tarehe tofauti na Roy Moore, mwendesha mashitaka wa wakati huo, walipokuwa na umri wa miaka 18 au chini ya umri huo. Walisema hapakua na mawasiliano ya kingono lakini wengi walisema walifumbatiwa kifuani.

Siku ya Jumatatu Novemba 13, mwanamke mwingine, mwenye umri wa miaka 55, Beverly Nelson, alisema katika mkutano na vyombo vya habari mjini New York kuwa Roy Moore alimdhalilisha kingono usiku mmoja wa mwezi Januari 1978 akiwa na umri wa miaka 16. Alisema alijaribu kumbaka katika gari lake.

Kwa mujibu wa mwanamke huyu, ambaye alikuwa mhudumu kwenye mgahawa wa Gadsden, Alabama, Roy Moore ghafla alimshika shingoni kwa kujaribu kumlazimisha wafanye tendo hilo.

Beverly Nelson alisema alijaribu kukabiliana na hali hiyo kabla ya hakimu huyo wa zamani, aliyekuwa wakati huo na umri wa 30, kuachana na nia yake.

"Wewe ni mtoto," Bw Moore alimwambia binti huyo kabla ya kumruhusu aende. "Mimi ni mwanasheria wa kaunti ya Etiwah, na ukithubutu kumwambia yeyote, hakuna mtu atakuamini."