MAREKANI-ISRAEL-PALESTINA

UN: Baraza la usalama kupiga kura kuzuia uamuzi wa Marekani kuhusu Jerusalem

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. REUTERS/Brendan McDermid

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa hii leo linatarajiwa kupigia kura azimio ambalo huenda likakataa uamuzi wa rais wa Marekani Donald Trump kutambua mji wa Jerusalem kama makao makuu ya nchi ya Israel.

Matangazo ya kibiashara

Nchi ya Misri ndiyo iliyoomba kufanyika kwa kura hiyo hapo jana ikiwa ni siku moja tu toka iwasilishe maazimio ambayo hata hivyo huenda yakapingwa kwa kura ya turufu na Marekani.

Akivunja na kutupilia mbali makubaliano ya jumuiya ya Kimataifa, rais Trump mwanzoni mwa mwezi huu alitangaza kuwa nchi yake itautambua mji wa Jerusalem kama makamo makuu ya Israel na kwamba itahamisha ubalozi wake kutoka mjini Tel-Aviv, tangazo lililosababisha maandamano kwenye nchi za mashariki ya kati.

Katika nyaraka iliyoonwa na shirika la habari la AFP, inaonesha kuwa Misri inataka suala ya Jerusalem litatuliwe kwa njia ya mazungumzo na kueleza masikitiko kutokana na uamuzi wa Marekani.

Nchi ya Israel ilikalia eneo la magharibi mwa Jerusalem mwaka 1967 wakati wa vita ya mashariki ya kati na kuchukua maeneo yote ya Jerusalem ikisema ni mji wake huku mamlaka ya Palestina ikisema eneo la Magharibi ni mji wake.

Nchi nyingi duniani zimejitokeza hadharani kupinga tangazo la Marekani walilosema litachochea kuchelewa kupatikana kwa suluhu kati ya Palestina na Israel.

Jumuiya ya kimataifa inataka kutambuliwa kwa suluhu ya uwepo wa mataifa mawili katika mji mmoja.