MAREKANI-UHAMIAJI-USALAMA

Trump aonya tishio la uhamiaji kwa usalama wa taifa

Donald Trump ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwazuia wahamiaji kwa maslahi ya taifa la Marekani.
Donald Trump ameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwazuia wahamiaji kwa maslahi ya taifa la Marekani. REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump amesema mfumo wa sasa wa uhamiaji nchini humo, unahatarisha usalama wa nchi yake. Kauli hii imekuja baada ya Trump kutoa matamshi tata kuhusu mataifa ya Afrika, ambayo wahamiaji wake wanaendelea kukimbilia nchini Marekani.

Matangazo ya kibiashara

Trump sasa anataka Mahakama ya Juu kumsaidia kudhibiti wahamiaji wanaoingia nchini humo, kwa kile anachosisitiza kuwa hii njia mojawapo ya kushinda ugaidi nchini mwake.

Mapema wiki hii rais Donald Trump kwa mara nyingine, alisema alieleweka vibaya baada ya kutumia neno shimo la choo, kuelezea mataifa ya Afrika.

Trump amesema, madai hayo yanarejesha nyuma juhudi za kufikia mwafaka wa kuwatambua na kuwasaidia wahamiaji walio na nia njema wanaokwenda Marekani.

Aidha, alimshutumu Seneta wa chama cha upinzani cha Democratic Dick Durbin kwa kuanza kusambaza habari za uongo kuwa alikuwa ametumia lugha ya kibaguzi alipokutana na wabunge kujadilia masuala ya wahamiaji.

Rais wa Marekani ameendelea kukosolewa ulimwenguni kwa kutumia lugha mbaya na hatua zake ambazo zinaonekana kuwatenga baadhi ya raia kutoka mataifa mbalimbali.

Wadadisi wanasema Donald Trump ni rais wa kwanza wa Marekani, ambaye kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja hatua zake zimepata upinzani mkubwa na hata kufutiliwa mbali katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo.