CUBA-HAKI

Kifungua mimba wa Fidel Castro ajiua Cuba

Makaburi ya Santa Ifigenia, alikozikwa Fidel Castro karibu na wanamapinduzi wenzanke.
Makaburi ya Santa Ifigenia, alikozikwa Fidel Castro karibu na wanamapinduzi wenzanke. © RFI/Véronique Gaymard

Mwana wa Aliyekuwa rais na mwanamapinduzi wa Cuba Fidel Castro, Fidel Ángel Castro Díaz-Balart, amejitoa uhai mjini Havana. Kwa mujibu wa mashahidi Castro Díaz-Balart alipatikana akiwa amefariki siku ya Alhamisi asubuhi.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa gazeti la serikali, Granma, Fidel Castro Diaz-Balart, aliyekuwa ametibiwa na kundi la madaktari kwa miezi kadha kutokana na msongo wa mawazo, alijitoa uhai asubuhi hii,

Tangazo kwenye televisheni limesema mazishi yake yatapangwa na familia yake, lakini maelezo zaidi hayakutolewa.

Castro Díaz-Balart, mwenye umri wa miaka 68, ambaye alifahamika kwa jina la “Fidelito" kutokana na kufanana sana na babake, alikua kifungua mimba wa rais Fidel Castro.

Kufikia wakati wa kifo chake, alikuwa mshauri wa kisayansi wa Baraza la Serikali ya Cuba na alihudumu kama makamu rais wa Chuo cha Sayansi cha Cuba.

Rais Fidel Castro alifariki dunia Novemba 2016 kwa maradhi ya muda mrefu baada ya kukabidhi madaraka kwa ndugu yake Raul Castro.