MAREKANI-USALAMA-MAUAJI

Watu 17 wauawa katika shambulio la risasi Marekani

Kikosi cha Zima Moto karibu na shule ya upili ya Marjory Stoneman Douglas huko Parkland, baada ya shambulio la risasi mnamo Februari 14, 2018.
Kikosi cha Zima Moto karibu na shule ya upili ya Marjory Stoneman Douglas huko Parkland, baada ya shambulio la risasi mnamo Februari 14, 2018. Instagram/@Dann_Edu/via REUTERS

Watu 17 wameuawa katika shambulio la risasi lililoendeshwa na kijana mmoja katika shule moja kusini mashariki mwa Florida. Shambulio hilo lilitokea jana Jumatano. Lakini mshambuliaji alikamatwa.

Matangazo ya kibiashara

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa amejihami kwa bunduki ya kisasa, alianza kushambulia bila ya mpangilio nje ya shule hiyo kabla ya kushambulia ndani.

Video fupi iliyorekodiwa na mwanafunzi mmoja wakati wa shambulio hilo, na ambayo ilirushwa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha vijana wakihangaika kwa lengo la kujificha chini ya madawati. Shambulio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya kumalizika kwa visomo katika shule ya upili ya Marjory Stoneman Douglas huko Parkland. Kwa mujibu wa ripoti ya awali, mshambuliaji aliua watu 17, wawili kati yao walifariki hospitali kutokana na majeraha walioyapata.

Mshambuliaji alikamatwa, jambo ambalo si la kawaida katika matukio kama hayo. Washambuliaji au wahusika katika matukio kama haya mara nyingi wanauawa kwa kupigwa risasi na polisi au wanaamua kujiua.

Kwa mujibu wa polisi, mtuhumiwa huyo ametajwa kwa jina la Nikolaus Cruz mwenye umri wa miaka 19 na kwamba alikuwa mwanafunzi katika shule hiyo aliyoishambulia.