BRAZIL-USALAMA

Wafungwa wawashikilia mateka wafanyakazi wa gereza mjini Rio de Janeiro

Polisi wakipiga kambi wakati wa operesheni dhidi ya wafanyabiashara wa madawa ya kulevya katika kitongoji cha Cidade De Deus, Rio de Janeiro, Brazil mnamo 1 Februari 2018.
Polisi wakipiga kambi wakati wa operesheni dhidi ya wafanyabiashara wa madawa ya kulevya katika kitongoji cha Cidade De Deus, Rio de Janeiro, Brazil mnamo 1 Februari 2018. REUTERS/Ricardo Moraes

Hali ya sintofahamu inaendelea katika gereza la Japari katika mji wa Rio de Janeiro, nchini Brasil, baada ya wafungwa kuchukua udhibiti wa gereza hilo huku wakiwashika mateka baadhi ya wafanyakazi.

Matangazo ya kibiashara

Ghasia hizo zinatokea siku mbili baada ya Rais wa Brazil Michel Temer, kusaini sheria ya kuwapa wanajeshi ruhusa ya kusimamia usalama wa mji wa Rio de Janeiro.

Maafisa wa gereza wanasema ghasia hizo huenda zimechangiwa na hatua mpya za ulinzi.

Tayari kikosi maalumu cha polisi kimelizingira jela hilo, huku ikipotiwa kuwa wafungwa watatu ambao walihusika katika kulidhibiti gereza hilo wamepigwa risasi lakini hawajapata majeraha ya kuwatishia maisha.

Mashahidi wanasema gereza hilo la Japari, lenye msongamano wa wafungwa liko chini ya udhibiti wa kundi moja la wahalifu lenye guvu zaidi na ambalo limekua likipambana na vijosi vya usalama katika mji wa Rio de Janeiro.

Chanzo cha polisi kinasema kuwa kundi hilo huenda lina lengo la kuwatorosha baadhi ya wanachama wake wanaoshikiliwa kwa makosa ya biashara haramu ya madawa ya kulevya.

Katikati ya mwezi Januari mwaka huu wafungwa wa gereza kuu la Alcaçuz katika jimbo la Rio Grande do Norte walichukua udhibiti wa gereza hilo, Wakati huo zaidi ya wafungwa kumi waliuwawa baadhi yao kwa kukatwa katwa katika makabiliano makali kati ya magenge hasimu katika gereza hilo.

Mapema mwezi Januari 2017 genge moja la uhalifu linaloendesha shughuli zake katika magereza mbalimbali nchini Brazil, liliwakata vichwa takriban wafungwa 33 katika gereza moja katika jimbo la Kaskazini la Roraima.

Maafisa wa Serikali wanasema ghasia hizo ni sehemu ya juhudi za magenge kuwa na mamlaka katika baadhi ya magereza.