KOREA KASKAZINI-MAREKANI

Korea Kaskazini yasema iko tayari kuzungumza na Marekani

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un KCTV / AFP

Korea Kaskazini inasema iko tayari kuzungumza na Marekani kuhusu masuala ya mradi wake wa nyuklia.

Matangazo ya kibiashara

Hakikisho hili limetolewa na rais wa nchi jirani ya Korea Kusini Moon Jae-in, wakati wa kufungwa kwa Michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi mjini Pyengchang.

Rais Moon mapema hivi leo alikutana na ujumbe wa Korea Kaskazini, ukiongozwa na kiongozi wa ujumbe wa Korea Kaskazini Kim Yong Chol.

Hii sio mara ya kwanza, kwa Korea Kaskazini kusema kuwa iko tayari kuzungumza na Marekani bila masharti yoyote, lakini Marekani imekuwa ikisema itaamini tu iwapo Pyongyang itaachana na mradi wake wa nyuklia na kujaribu silaha zake za maangamizi.

Wakati wa kuanza kwa michezo hii ya Olimpiki mapema mwezi huu na kuhudhuriwa na Makamu wa rais wa Marekani Mike Pence, mwakilishi huyo wa Marekani hakusalimiana na ujumbe wa Korea Kaskazini ishara ilionesha kuwa, uhusiano wa mataifa hayo mawili ni mbaya.

Korea Kaskazini na Marekani katika siku za hivi karibuni, yamekuwa yakitishiana kushambuliana.

Marekani imekuwa ikiongoza harakati za kuiwekea vikwazo vya kibiashara Korea Kaskazini.