FACEBOOK-MAREKANI

Hisa za Facebook zaporomoka kwa kashfa ya kutumia vibaya takwimu za wateja wake

Picha ya maktaba kuhusu Facebook
Picha ya maktaba kuhusu Facebook REUTERS/Dado Ruvic/Illustration/File Photo

Bei ya hisa za kampuni ya mtandao wa kijamii wa Facebook imeendelea kuporomoka wakati huu uongozi wake ukikosolewa ndani na nje ya nchi kutokana na kuibuka taarifa kuwa kampuni iliyofanya kazi na timu ya kampeni ya rais Donald Trump iliwekeza na kutumia vibaya takwimu za watumiaji wa mtandao huo zaidi ya milioni 50.

Matangazo ya kibiashara

Wito wa kufanyika uchunguzi umetoka kutoka kila pande za dunia baada ya kampuni ya Facebook kujibu tuhuma za ripoti kuwa ilitumia vibaya takwimu zake kwa kuifunga akaunti ya kampuni ya Cambridge Analytica, kampuni ya kiingereza iliyokuwa imekodiwa na timu ya Trump wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016.

Seneta wa chama cha Democratic Amy Klobuchar na mwenzake wa Republican John Kennedy wamemtaka mkurugenzi na mmliki wa mtandaio wa Facebook Mark Zuckerberg kujiwasilisha mbele ya baraza la Congress sambamba na mkurugenzi wa Google na Twitter.

Wabunge hao wanadai kuwa mitandao hiyo kwa kiwango kikubwa ilitumia vibaya takwimu binafsi za wateja wake na kukosoa umakini wa uangalizi na kuibusha wasiwasi kuhusu kuaminika kwa uchaguzi wa Marekani pamoja na haki ya usiri.

Mkuu wa masuala ya usalama wa Facebook Alex Stamos amesema kazi yake imebadilika na kujikita zaidi katika masuala ya hatari ya kiusalama yanayoibuka.

Stamos amesema amebadili kazi yake baada ya ripoti ya gazeti la New York Times kudai kuwa alikuwa aache kazi kwenye kampuni hiyo kutokana na mvutano wa ndani kuhusu namna watakavyoshughulikia suala hili.