URUSI-MAREKANI

Urusi yawafukuza wanadiplomasia 60 wa Marekani

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrovn wakati akitangaza kufukuzwa kwa wanadiplomasia 60 w Marekani. 29 Machi 2018.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrovn wakati akitangaza kufukuzwa kwa wanadiplomasia 60 w Marekani. 29 Machi 2018. REUTERS/Sergei Karpukhin

Nchi ya Urusi, nayo imetangaza kuwafurusha mamia ya wanadiplomasia wa Marekani na kuagiza kufungwa kwa ofisi za ubalozi mjini Saint Petersburg katika kile kinachoonekana ni kujibu mapigo kutokana na hatua zilizochukuliwa na nchi za Magharibi kuitenga Serikali ya Moscow kutokana na tuhuma kuwa ilihusika katika shambulio la sumu dhidi ya jasusi wake wa zamani.

Matangazo ya kibiashara

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema nchi yake itawafukuza nchini humo wanadiplomasia 60 wa Marekani na kufunga ofisi za ubalozi wake mjini Saint Petersburg kujibu kitendo cha wanadiplomasia wake kufukuzwa na nchi za Magharibi.

Utawala wa Washington wenyewe umesema kuwa kitendo kilichofanywa na Urusi hakina msingi wowote na kwamba Serikali inafikiria hatua nyingine za kuchukua.

“Ni wazi kutokana na orodha tuliyokabidhiwa kuwa Urusi haiko tayari kwa mazungumzo ya masuala yanazozikabili nchi hizi mbili,” amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nje Heather Nauert.

“Nataka niwakumbushe kuwa hakuna maelezo yoyote ya msingi yanayoweza kutolewa na Urusi kuhusu uamuzi wake. Uamuzi wetu ulizingatia kile ambacho kilitokea jijini London.”

Msemaji wa ikulu Sarah Sanders amesema uamuzi wa Urusi kuwafurusha wanadiplomasia wake kunatoa ishara ya kuendelea kuzorota kwa uhusiano wa nchi hizo mbili huku akitetea uamuzi wa nchi yake na ule wa mataifa ya magharibi.

Waziri Lavrov amesema kuwa balozi wa Marekani nchini Urusi Jon Huntsman ameshapewa taarifa kuhusu hili na kwamba kama ilivyokuwa kwa idadi ya wanadiplomasia wa Urusi waliofukuzwa ndivyo itakuwa kwa wanadiplomasia wake.