MAREKANI-IRAN-NYUKLIA-USALAMA

Washington kutangaza uamuzi wake kuhusu mpango wa nyukilia wa Iran

Rais wa Marekani Donald Trump, Mei 7, 2018 katika ikulu ya White House.
Rais wa Marekani Donald Trump, Mei 7, 2018 katika ikulu ya White House. REUTERS/Kevin Lamarque

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajia kutangaza Jumanne wiki hii uamuzi wake kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Rais Trump ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa yuko tayari kuchukua uamuzi Jumanne wiki hii.

Matangazo ya kibiashara

Licha ya wito kutoka jumuiya ya kimataifa, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, wataalam wanaamini kuwa rais wa Marekani anajiandaa kutangaza kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa Vienna, uliyosainiwa mwaka 2015 kati ya kundi "5 1" na Iran.

Wakati wa ziara yake huko Washington mwishoni mwa mwezi Aprili, Emmanuel Macron alijaribu kumshawishi Donald Trump asiiondoi Marekani katika mpango huo. Rais wa Ufaransa aliutaja mkataba huo kuwa ni kamilifu, lakini bila mbadala bora.

Katika ziara yake, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimmuomba rais wa Marekani kutochukua hatua ya kujiondoa kwenye mkataba wa Vienna. Hatimaye, Jumatatu wiki hii hii, ilikuwa zamu ya Boris Johnson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, kumuomba rais wa Marekani kutochukua hatua hiyo.

Pamoja na wito huu kutoka London, Berlin na Paris, wanadiplomasia na wataalam wanaamini kwamba Donald Trump anajiandaa kutangaza kujiondoa kwenye makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Irani yaliyosainiwa mjini Vienna mwaka 2015 baada ya miaka kumi na mbili ya mazungumzo na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa .

Makubaliano hayo yanaondoa vikwazo dhidi ya Iran kwa kubadilishana na ahadi kuhusu mpango wake wa nyuklia. Donald Trump mara kwa mara amekua akirejelea kauli yake hiyo ya kujiondoa kwenye mkataba huo. Anaoona mpango huo wa hatua za pamoja kuwa ni "mbaya." Anaona kuwa mpango huo ni "mbaya zaidi" kuwahi kujadiliwa na Marekani.

Robert Malley, afisa wa marekani aliyeiwakilisha nchi hiyo katika mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran wakati wa utawala wa Barack Obama, anasema kujiondoa kwa Marekani kwenye mkataba huo, kuna hatari ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Marekani na Iran, kuna uwezekano wa Iran kujejelea mpango wake wa nyuklia na uwezekano wa makabiliano ya kijeshi kati ya nchi hizi mbili.

"Madhara makubwa, yatajitokeza katika siku, wiki na miezi, na pengine miaka ijayo na kuongezeka kwa mvutano kati ya Marekani na Iran, " amesema Robert Malley, mkurugenzi wa shirika la International Crisis Group na mshauri wa zamani wa Barack Obama kuhusu Ghuba ya Uajemi.