MAREKANI-VENEZUELA-VIKWAZO-SIASA

Marekani yawekea Venezuela vikwazo vipya

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro wakati akitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais, Mei 20, 2018 Caracas.
Rais wa Venezuela Nicolas Maduro wakati akitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais, Mei 20, 2018 Caracas. REUTERS/Carlos Garcia Rawlin

Marekani imeiwekea Venezuela vikwazo vipya vya kifedha, siku mbili baada ya Rais Nicolas Maduro kuchaguliwa kwa mara nyingine. Uchaguzi huo ulipingwa na upinzani pamoja na jumuiya ya kimataifa baada ya upinzani kuamua kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho cha urais.

Matangazo ya kibiashara

Maduro atasalia madarakani hadi mwaka 2025. Hali hiyo inaendelea kusababisha Venezuela kutengwa kwenye ngazi ya kimataifa. Venezuela inakabiliwa na mgogoro wa kisiasa na kiuchumi.

Rais wa Marekani Donald Trump amesaini sheria inayolenga kupunguza uwezo wa serikali ya Caracas kuuza mali zake. Makamu wa Rais Mike Pence aliuita uchaguzi huo kuwa ni "mchezo".

Kwa upande mwingine, Rais wa Urusi Vladimir Putin amekaribisha ushindi wa Maduro na kumpongeza, akimtakia "afya njema na mafanikio katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi zinazoikabili nchi yake". Cuba pia imekaribisha "ushindi mkubwa" wa kiongozi wa Venezuela, ikimhakikishia kumuunga mkono na kutoa msaada wake.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter, Rais Nicolas Maduro amemshukuru Vladimir Putin kwa kutambua ushindi wake, Rais wa Jamhuri ya China Xi Jinping kwa ujumbe wake wa kupongeza ushindi "mkubwa" pamoja na viongozi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Nicaragua Daniel Ortega.

Katika uchaguzi uliokosolewa na jumuiya ya kimataifa na kususiwa na wapinzani, Bw Maduro, mwenye umri wa miaka 55, alishinda kwa 68% ya kura dhidi ya 21.2% alizopata mpinzani wake mkuu Henri Falcon, mwenye umri wa miaka 56.