BRAZIL-SIASA-USALAMA

Mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi achomwa kisu Brazil

Ikiwa umsalia mwezi mmoja kabla ya duru ya kwanza ya uchaguzi wa urais nchini Brazil, kumetokea hali ya taharuki nchini humo baada ya mgombea mkuu anayepewa nafasi kubwa ya kushinda uchaguzi huo kuchomwa kisu.

Jair Bolsonaro, ajeruhiwa kwa kisu Septemba 6, 2018 huko Juiz de Fora, wakati wa kampeni ya uchaguzi.
Jair Bolsonaro, ajeruhiwa kwa kisu Septemba 6, 2018 huko Juiz de Fora, wakati wa kampeni ya uchaguzi. Raysa LEITE / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mgombea urais wa mrengo wa kulia Jair Bolsonaro, alichomwa kisu Alhamisi wiki hii wakati wa mkutano wake wa kampeni ya uchaguzi katika mji wa Juiz de Fora, katika Jimbo la Minas Gerais. alifanyiwa upasuaji na anaweza kuhamishiwa katika hospitali ya Sao Paulo leo Ijumaa. Hali yake ya afya inaendelea vizuri.

Wapinzani wengi wa Jair Bolsonaro, kutoka mrengo wa kulia na ule wa kushoto, wamelaani shambulio hilo la siku ya Alhamisi usiku, na wameonyesha mshikamano wao dhidi ya kile walisema kitendo cha ujinga na kisiokubalika.

Mgombea huyo wa mrengo wa kulia alichomwa kisu katika mkutano mkubwa wenye mkusanyiko wa watu wengi katika eneo la kusini mashariki.

Mwanasiasa huyo ambaye amekua gumzo kwa maoni yake kuhusu ubaguzi wa rangi, amepata kura nyingi katika kura za maoni za hivi karibuni.

Wauguzi wa hospitali walisema kuwa Bw Bolsonaro amepata jeraha kubwa na limechimba sana kwenye utumbo lakini sasa anaendelea vizuri.

Alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa muda wa masaa baada ya upasuaji, lakini atasalia hospitali hadi siku kumi.

Mshukiwa wa kitendo hicho, Adelio Obispo de Oliveira, anashikiliwa na polisi, kwa mujibu wa chanzo cha polisi.