Lula aapa kuendelea kupambana dhidi ya uamuzi wa mahakama
Imechapishwa:
Rais wa zamani wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 12 kwa madai ya rushwa tangu mwezi Aprili, ataendelea na vita yake ya kisheria ili arejeshewe haki ya kuwania katika uchaguzi wa urais mwezi ujao, wanasheria wake wamesema.
Tangazo hili linakuja wakati chama chake cha PT, kimepewa hadi Jumanne usiku kuteua mgombea mwengine kuchukua nafasi ya Lula kuelekea uchaguzi wa Oktoba 7.
Mwishoni mwa mwezi Agosti, Mahakama Kuu ya Uchaguzi ilitangaza kwamba Lula hana vigezo kisheria vya kuwania katika uchaguzi wa urais.
Siku ya Jumatatu wanasheria wa Lula na Fernando Haddad, mgombea mwenza, walimtembelea Lula katika jela wanakozuiliwa.
Vyanzo vya chama cha PTvimebaini kwamba katika mazungumzo yao Lula alitakiwa kumruhusu Haddad kuwania kwenye nafasi yake na kumpa barua ambapo anawatolea wito wawafuasi wake kumpigia kura.