MAREKANI-ICC-HAKI-UCHUMI

Marekani yaishambulia kwa maneno makali ICC

Balozi wa zamani na mtangazaji wa zamani wa Fox News, John Bolton ni mshauri wa usalama wa kitaifa wa Donald Trump.
Balozi wa zamani na mtangazaji wa zamani wa Fox News, John Bolton ni mshauri wa usalama wa kitaifa wa Donald Trump. REUTERS/Denis Balibouse

Marekani kupitia Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House, John Bolton, imeishambulia kwa maneno makali Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Matangazo ya kibiashara

Marekani imetoa vitisho kwa majaji na waendesha mashitaka wa ICC kuwachukulia vikwazo ikiwa wataifungulia mashitaka nchi hiyo, Israeli au washirika wake wengine.

John Bolton hapendi ICC na ametoa kauli hiyo kwa niaba ya "rais wa Marekani". John Bolton, ambaye ni Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House ameihutumu Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwamba " sio halali", lakini pia "haiwajibiki, haina mamlaka yoyote na ni chombo hatari."

"Ikiwa Mahakama itashambulia Marekani, Israeli au washirika wengine wa Marekani, hatutasalia kimya." Marekani haikutia saini kwenye Mkataba wa Roma. Wakati huo huo balozi wa zamani wa Marekani katika Umoja wa Mataifa anaogopa uwezekano wa uchunguzi kubaini iwapo makosa ya uhalifu wa kivita yalitekelezwa na wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan au kuanzishwa uchunguzi dhidi ya Israel.

John Bolton alitangaza, kwa kutisha, kwa vikwazo ambavyo Marekani inaweza kuchukua kwa kulipiza kisasi: "Tutapiga marufuku majaji na waendesha mashitaka wa ICC kuingia Marekani. Tutachukua vikwazo dhidi ya mali zao katika mfumo wa kifedha wa Marekani, na tutachukua hatua za kisheria dhidi yao katika mfumo wetu wa mahakama. "

Kwa hali yoyote ile, serikali ya Marekani "haitashirikiana na ICC, wala kutoa msaada wowote, hakuna kujiunga na ICC, " amesema John Bolton.

Marekani ilituma wanajeshi wake nchini Afganistan mwaka 2001 kupambana na kundi la Taliban na kufikia mwaka 2016 idadi kubwa ya wanajeshi walirejea nyumbani.