MAREKANI-KAVANAUGH

Kavanaugh: Bunge la seneti lajiandaa kumpitisha mteule wa Trump

Jaji Brett Kavanaugh wakati akihojiwa kwenye moja ya vikao vya kamati ya sheria bunge la seneti
Jaji Brett Kavanaugh wakati akihojiwa kwenye moja ya vikao vya kamati ya sheria bunge la seneti ©Gabriella Demczuk/REUTERS

Bunge la Seneti nchini Marekani hii leo linatarajiwa kumuidhinisha mteule wa rais Donald Trump, Brett Kavanaugh katika nafasi ya jaji wa mahakama ya juu, baada ya wabunge wawili wa Republican kuonesha nia ya kupiga kura ya ndio.

Matangazo ya kibiashara

Ikiwa wabunge hawa watamudhinisha jaji Kavanaugh kwenye nafasi hiyo, utakuwa ni ushindi mkubwa kwa rais Trump ambaye anataka jaji ambaye atatetea mipango yake.

Seneta wa Republican Susaz Collins ambaye awali alionesha kutounga mkono uteuzi wa Kavanaugh, ametangaza kuwa atapiga kura ya ndio, sambamba na seneta wa chama cha Democrats Joe Machin anaekosolewa pakubwa na wafuasi wake.

Uamuzi wa maseneta hawa wawili unafanya idadi ya wabunge waliotangaza kupiga kura ya ndio kumidhinisha Kavanaugh kufikia 51 katika bunge lenye watu 100.

Juma moja lililopita kamati ya sheria ya bunge iliridhia kusitisha kwa muda zoezi la upigaji kura kuridhia au kutoridhia uteuzi wa Kavanaugh baada ya mwalimu mmoja wa chuo kikuu kujitokeza na kudai kuwa aliwahi kudhalilishwa kingono na mteule huyo.

Tuhuma hizi zilisababisha mijadala mikali nje na ndani ya kamati ya sheria ambapo wabunge kutoka pande mbili walituhumiana kwa kusimamia maslahi ya kisiasa katika kuamua kuhusu suala la Kavanaugh.

Waandamanaji wakiwa na mabango kupinga uteuzi wa jaji Brett Kavanaugh
Waandamanaji wakiwa na mabango kupinga uteuzi wa jaji Brett Kavanaugh Eric BARADAT / AFP

Baadae rais Trump aliagiza kufanyika kwa uchaguzi zaidi uliofanywa na shirika la upelelezi la FBI, ambapo liliwahoji wanawake kadhaa walioripoti kufanyiwa vitendo hivyo na Kavanaugh.

Hata hivyo juma hili taarifa ya FBI iliyowasilishwa kwenye kamati ya sheria haikupendekeza kufunguliwa mashtaka kwa jaji Kavanaugh, taarifa ambayo ilikuwa pigo kwa wabunge wa Democrats ambao tangu awali walipinga uteuzi wake.

Ikiwa ataidhinishwa, Kavanaugh atakuwa kiungo muhimu katika serikali ya rais Trump hasa pale atakapowasilisha masuala yake katika mahakama ya juu au pale itakapotokea watu kupinga maamuzi yake katika mahakama ya juu ambapo jaji Kavanaugh anatarajiwa kuzuia jariibo lolote la kumuondoa madarakani rais Trump.

Licha ya maandamano mfululizo kushinikiza wabunge hao kutopiga kura ya ndio kumidhinisha Kavanaugh, ni wazi kila dalili zinaonesha kuwa wabunge hao sasa watamuidhinisha kutokana na uwingi wa idadi ya wabunge wa Republican.

Rais Trump amewashutumu wanawake waliomtuhumu jaji Kavanaugh kwa udhalilishaji wa kingono huku akiwaita waandamanaji wanaipiga uteuzi wake kama mamluki waliopewa fedha kuwatisha wabunge.

Huu ulikuwa mchakato wa uteuzi tata uliowahi kufanywa na rais Trump na kusababisha mvutano mkali katika kamati ya sheria ambayo ilitumia majuma kadhaa kuvutano kuhusu jaji Kavanaugh.

Jaji anayeteuliwa kuhudumu katika mahakama ya juu nchini Marekani, huudumu katika kipindi cha maisha yake yote.