MAREKANI-URUSI-NYUKLIA-USALAMA

Donald Trump: Marekani iko tayari kuanza kutengeneza silaha

Rais wa Marekani Donald Trump  akiwa katika kampeni Missoula, katika eneo la Montana, Oktoba 18, 2018.
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa katika kampeni Missoula, katika eneo la Montana, Oktoba 18, 2018. REUTERS/Jonathan Ernst

Siku chache baada ya kutangaza kujitoa kwenye mkataba wa nyuklia na nchi ya Urusi, rais wa Marekani Donald Trump amesema nchi yake kwa sasa itaanza kutengeneza upya silaha zake za maangamizi.

Matangazo ya kibiashara

Wakati huu ambapo matamshi yake yamezusha wasiwasi kidunia na kusababisha ukosolewaji mkubwa, rais Trump sasa ameenda mbali zaidi na kutangaza kuwa nchi yake inastahili kuwa na silaha ambazo Urusi na China inazo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, rais Trump ametetea uamuzi wa nchi yake kujitoa kwenye makubaliano hayo, akisema wakati nchi yake ikiwa haitengenezi silaha za maangamizi, wenzao Urusi na China wameendelea kufanya majaribio ya silaha za masafa marefu.

Wataalamu wa masuala ya usalama wanaona kuwa uamuzi wa Marekani unahatarisha usalama wa dunia hasa wakati huu nchi hiyo ikiwa mstari wa mbele kulazimisha nchi kadhaa kuachana na urutubishaji wa Uranium.