MAREKANI-SAUDI ARABIA-KHASHOGGI

Trump asema Saudi Arabia ilikosea kulinda mauaji ya Khashoggi

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald Trump Reuters

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki alikuwa mkali sana kuhusu Serikali ya Saudi Arabia katika hotuba yake ambayo aliitumia kueleza namna utawala wa Riyadh ulivyopanga mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Matangazo ya kibiashara

Rais Trump amesema nchi ya Saudi Arabia ilikosea sana katika kujaribu kuficha ukweli wa kile kilichomtokea mwandishi wa habari Khashoggi alipotembelea ubalozi wa nchi yake jijini Istanbul.

Aidha, Maekani imetangaza kuwa maafisa wa Saudi Arabia 21 waliodaiwa kuhusika, hawataruhusiwa kuzuru Marekani.

Matamshi ya Trump yamekuja wakati huu mkurugenzi wake wa shirika la ujasusi la CIA akiwa nchini Uturuki kupata ukweli zaidi kuhusu Mwanahabari huyo aliyekuwa mkaazi wa Marekan.

Siku ya Jumanne, rais Erdogan aliwaambia wabunge kuwa Saudi Arabia ilipanga kwa muda mrefu mauaji ya Khashoggi, aliyekuwa anaandika makala katika Gazeti la Marekani la Washington Post, kuukosoa uongozi wa Kifalme katika nchi yake.

Ni mauaji yaliyoshutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa, wakati huu uongozi wa Riyadh ukisema haukuwa na taarifa ya kuuawa kwa mwanahabari huyo.

Mwili wake bado haujabainika uko wapi.