Donald Trump amfuta kazi mwanasheria mkuu Marekani
Imechapishwa:
Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Marekani, Jeff Sessions, amefutwa kazi na rais Donald Trump, hatua inayozidisha wasiwasi kuhusu uwezekano wa kiongozi huyo kusimamisha uchunguzi unaoendelea ikiwa Urusi iliingilia uchaguzi mkuu uliyopita.
Uamuzi huu umekuja baada ya karibu mwaka mmoja wa lawama kutoka kwa rais Trump aliyekuwa akimtuhumu Sessions kwa kujitoa katika kuhusika na uchunguzi kuhusu nchi ya Urusi kuingilia uchaguzi wa mwaka 2016, hatua iliyopelekea kuundwa kwa tume maalumu inayoongozwa na Robert Mueller.
Rais Trump alitangaza uamuzi wa kumfuta kazi Sessions kupitia ukurasa wake wa Twitter, ambapo amemshukuru kwa muda aliokuwa ofisini huku akimteua aliyekuwa mnadhimu wa Sessions, Matthew Whitaker kusimamia uchunguzi huo.
Hata hivyo uteuzi wa Whitaker umeibua sintofahamu zaidi kutokana na msimamo wake kuhusu tume inayoongozwa na Mueller ambapo wakati wote wa uchunguzi ukiendelea, alikuwa anaukosoa na kutaka tume hiyo kuvunjwa.
Tayari upinzani unamtaka Whitaker kujiweka kando na uchunguzi huo kutokana na matamshi aliyowahi kuyatoa.