G20: Donald Trump afuta mkutano wake na Vladimir Putin
Imechapishwa:
Kabla ya kuanza kwa mkutano wa G20 huko Argentina, rais wa Marekani Donald Trump amefuta ghalfa mkutano wake uliopangwa kufanyika Jumamosi, Desemba 1 na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin.
Katika Ukurasa wake wa Twitter Donald Trump anamshtumu Vladimir Putin kwa kutowaachilia huru askari wa kikosi cha wanamaji wa Ukraine nameli zao zilikamatwa karibu na Bahari ya Azov.
Hatua hiyo inakuja tu siku chache baada ya kufichuliwa taarifa mpya nchini Marekani katika uchunguzi kuhusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa urais nchini Marekani.
Katika mkutano huo Rais Donald Trump anatarajia kupambana na China katika biashara na kusisitiza maneno yake dhidi ya Urusi kuhusiana na Ukraine.
Mkutano huo utakaofanyika mwishoni mwa juma unakabiliwa na ongezeko la tahadhari ya juu, miongoni mwao kutoka Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF, kuhusiana na hatari inayoukabili uchumi wa dunia kutokana na vita ya kibiashara ya Trump.
Viongozi wa G20, ambao nchi zao zinachangia kiasi cha nne kwa tano ya uchumi wa dunia, zilikutana kwanza Novemba 2008 kuunda nguvu ya pamoja dhidi ya mzozo wa kifedha wa dunia.